Monday, August 4, 2008

Rais Kikwete atembelea Mradi wa
Makaa ya Mawa wa
Mchuchuma...
Rais Jakaya Kikwete akitazama makaa ya mawe alipotembelea Mradi wa Makaa hayo ya mawe wa Mchuchuma Coal Mine Mkoani Iringa jana.
----------
Na Mgaya Kingoba,Ludewa
Rais Jakaya Kikwete jana alitembelea mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na kuwaahidi wakazi wa Ludewa na taifa kwa ujumla,kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha mradi huo unakamilika katika siku za karibuni.Akihutubia wananchi baada ya kukagua mradi huo, Rais Kikwete alisema suala la mradi huo na ule wa chuma wa Liganga yamewekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)ya mwaka 2005/2010 na kwamba,masuala hayo yamekuwa ya muda mrefu,hivyo umefika wakati yatekelezwe.
Rais alisema kwa upande wa Mchuchuma, kazi ya utafiti imekamilika,anatafutwa mwekezaji na kwa Liganga utafiti unaendelea.“Kazi ya sasa ni kuona namna gani kutekeleza kazi hiyo ili tukamilishe haraka kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wa Ludewa na taifa kwa ujumla,” alisema Rais.
Alisema mradi wa Mchuchuma unatarajiwa kuzalisha tani milioni 500 na kwa upande wa Liganga ni tani 1,000,kiasi ambacho ni kikubwa na kitaleta msukumo mkubwa zaidi.
“Tulichoamua sasa ni kutafuta njia ya haraka ya kuendeleza miradi hiyo.Tatizo letu kubwa kuliko yote itakuwa namna gani ya kuhakikisha tunafikisha mazao hayo kwenye soko,” Rais Kikwete.Alisema,tatizo ni namna ya kujenga reli kutoka Mchuchuma inayotarajiwa kugharimu dola bilioni 1.6 za Marekani.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete,suala la kujenga barabara nalo ni gumu kwa sababu njia fupi zaidi ni kilomita 70 ambayo inapita katika milima na mabonde.“Dhamira yetu sisi kama wanadamu ni kwamba tusishindwe kwa hiyo katika muda si mrefu tutakuwa tumepata jawabu na kuanza kutekeleza miradi hii,”alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC),Gideon Nasari alisema uchunguzi kuhusu makaa ya mawe umekamilika na kwamba hivi sasa anatafutwa mwekezaji atakayekuwa mbia katika mradi huo.Nasari alisema mradi huo,mbali na kutarajiwa kuzalisha megawati 400 za umeme,pia unatarajiwa kuyeyusha chuma cha Liganga.
Alisema nafasi kwa ajili ya wazabuni kuomba kuwekeza katika mradi huo zimeshatangazwa,na tayari kampuni 50 za kimataifa zikiwamo kutoka China,Australia,Japan,India na Afrika Kusini zimetuma maombi.Kwa mujibu wa Nasari,zinahitajika dola za Marekani milioni 800 kwa ajili ya kujenga njia ya umeme kwenda katika gridi ya taifa,dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya kujenga miundombinu na ofisi.
Awali akizungumza katika eneo la mradi,Mkomang’ombe,Rais Kikwete aliagiza kuwa taratibu zifuatwe wakati wa kuhamisha wananchi kwenye eneo la mradi,kwa kuwa kuna watu wenye maeneo yao na wameishi hapo kwa muda mrefu.

No comments: