Kampuni ya Zain Yapata Mtoto
Aitwaye Zain..
----------
Na Mwandishi Wetu..
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zain Tanzania,imepata mtoto aitwaye Zain aliyezaliwa katika Hospitali ya Mwananyamala,Dar es Salaam usiku wa uzinduzi wa kubadilisha jina la Celtel kuwa Zain.Mtoto huyo,Zain Ally Sekondi alikuwa wa kwanza kuzaliwa hospitalini hapo muda mfupi baada ya saa 6.00 usiku wa Ijumaa Agosti Mosi,mwaka huu.
Alizaliwa na mama yake aitwaye,Shakilla Sekondi mwenye umri wa miaka 25.Kutokana na kuzaliwa kwa mtoto huyo,Kampuni ya Zain iliamua kumpa zawadi anuwai na inatarajia kufuatilia ukuaji wake na kuangalia maendeleo yake kwa ujumla.Akimkabidhi zawadi hospitalini hapo ikiwa ni pamoja na beseni lenye vifaa vya mtoto,Ofisa Habari wa Zain Tanzania, Celine Njuju alisema wamefurahishwa na kitendo cha mtoto huyo kupewa jina la Zain.
"Maana ya Zain ni kitu kizuri chenye kuleta furaha na ni matumaini yetu mototo huyu ataleta furaha kwa wazazi wake na jamii kwa ujumla,"alisema Celine.Mama wa mtoto huyo, Shakilla anayeishi eneo la Tandale,Dar es Salaam,alisema yeye na mumewe,Ally Sekondi na bibi wa mtoto huyo,Mwanahawa Kaziyabure,walifikia muafaka wa kumpachika mtoto huyo jina la Zain.Muuguzi Kiongozi wa wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo,Catherine Mbeyela aliishukuru Zain kwa uamuzi wake wa kutoa zawadi kwa mtoto huyo,na akaipongeza kwa kujitolea kutoa huduma nyingi za maendeleo kwa jamii hususan suala la elimu.
Zain ilibadilisha jina katika nchi zote 14 ambazo inafanya shughuli zake barani Afrika kutoka Celtel na kuwa Zain,Agosti 1,mwaka huu,katika tukio la kihistoria lililojumuisha wafanyakazi, vyombo vya habari na watu mashuhuri.Meneja Uhusiano wa Zain Tanzania,Beatrice Mallya alisema kama mtandao mmoja,Zain imejipanga vyema kutoa huduma nzuri kwa wateja wa Zain barani Afrika na Mashariki ya Kati.
“Zain kama mtandao uliosambaa sehemu mbalimbali duniani, inaamini huu ni mwanzo wa enzi mpya kwa wateja wa Zain Tanzania.Nembo mpya ya Zain ina rangi nyingi za kuvutia na imelenga kuhudumia wateja wa rika zote katika soko na kutoa zawadi kwa mtoto Zain ni sehemu ya huduma tutakazoendelea kutoa kwa jamii na wateja wetu.“Tunaamini wateja wetu wote na watu wengine Tanzania watajumuika nasi katika mabadiliko haya na kufurahia kauli mbiu yetu ya‘Wonderful World’Ulimwengu maridhawa inayowakilisha maisha mapya kwa wateja wetu.
“Kwa kuibadilisha Celtel kuwa Zain,tunachukua mafanikio ya Afrika na kuyasambaza sehemu mbalimbali duniani,”alisema Beatrice.Zain ni mtandao ulioenea katika nchi za Tanzania,Kenya, Uganda,Jamhuri ya Kongo,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Gabon,Zambia, Madagascar, Malawi,Niger,Nigeria,Sierra Leone,Burkina Faso na Chad.Zain pia itazindua huduma zake nchini Ghana baadaye mwaka huu wa 2008.
No comments:
Post a Comment