Saturday, August 2, 2008

Deus Mallya atinga kizimbani
Deus Mallya anayetuhumiwa kuwa dereva wa gari lililopata ajali na kusababisha kifo cha wangwe
juu mwili wa marehemu chacha wangwe ukitolewa hospitali ya wilaya ya tarime baada ya kufanyiwa uchunguzi wa pili na mtaalamu aliyeletwa na familia ya marehemu, kwa mujibu wa mdau jacob mugini aliyepiga picha hizi
ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya marehemu chacha wangwe wakisubiri matokeo ya uchunguzi wa sababu ya kifo cha wangwe nje ya hospitali ya wilaya ya tarime

DEUS Mallya (27) ambaye anatuhumiwa kuwa dereva wa gari lililopata ajali na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime Marehemu Chacha Wangwe Jumatatu usiku, jana alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuendesha gari kizembe na kuendesha gari bila kuwa na leseni.

Alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Dodoma, Mh. Moses Mzuma.

Mwendesha mashtaka, Mratibu Msaidizi wa polisi Polycarp Urio alidai mahakamani hapo kwamba Mallya alifanya makosa hayo Julai 28, 2008 eneo la Pandambili, kiasi cha kilomita 100 toka Dodoma, katika barabara kuu ya kuelekea Dar.

Mallya alikana mashtaka yote na amerejeshwa rumande hadi Agosti 14 kesi hiyo itaposikilizwa tena.

Utata mkubwa ulighubika ajali hiyo kutokana na madai tofauti ya nani alikuwa dereva wa gari hilo dogo. Mtuhumiwa alikana kwamba hakuendesha yeye, wakati mtoto wa marehemu Zakayo Chacha alidai ni yeye Mallya aliyekuwa dereva.

Utata huo uliepelekea kufanyika upya kwa uchunguzi wa kubaini sababu ya kifo cha Marehemu Wangwe, lakini mtaalamu aliyeletwa na familia ya marehemu alithibitisha kwamba kifo hicho hakikutokana na majeraha ya risasi kama ilivyokuwa ikidaiwa, bali kwa majeraha ya ajali hiyo.

Marehemu Chacha Wangwe hatimaye alizikwa jana huko Tarime, ikiwa ni baada ya mazishi yake kuahirishwa kwa siku moja ili kupisha uchunguzi wa kina ufanywe kwanza na mtaalamu huru aliyeletwa na familia.

No comments: