Friday, August 1, 2008

Acheni kuiba kura -Sumaye

WAZIRI Mkuu mstaafu,Frederick Sumaye Pichani,amebeza tabia ya kuiba kura na baadaye kuanzisha serikali ya mseto kama njia ya kuleta suluhu katika nchi.

Alisema tabia ya kuunda serikali ya mseto kama ilivyofanyika nchini Kenya na Zimbabwe na kama inavyopendekezwa kuwapo Visiwani Zanzibar kwa kushirikisha vyama vikuu vya upinzani,kutaua upinzani unaokusudiwa.

Sumaye alitoa kauli hiyo katika mahojiano yake maalumu na kipindi cha Jicho Letu wiki hii, kinachorushwa na kituo cha Radio Clouds cha jijini Dar es Salaam.Kipindi hicho kitarushwa hewani Jumamosi ijayo.

Alisema tabia ya kuiba kura na baadaye kuunda serikali ya mseto, inazidi kukua katika nchi za Afrika.

Alisema serikali za mseto zinazotakiwa ni zile zinazoanzishwa kwa makubalino tangu mwanzo kuwa chama kimoja kikishinda,kitaunda serikali ya mseto na chama fulani,lakini si mseto unaotokana na ugomvi wa kuiba kura.

‘Mseto wa Kiafrika,si mzuri.Serikali za mseto zinavyotakiwa ni pale ambapo pana demokrasia sahihi,unakuwa na vyama vya siasa,unakuwa na vyama ambavyo vinasema tangu mwanzo kuwa nikishinda, nikiunda serikali,nitakuchukua wewe,tutakuwa pamoja.

‘‘Serikali za mseto unaotengenezwa kwa mapambano kama Kenya na Zimbambwe ni mbaya kwa sababu unaua upinzani.Unachukua chama kimoja kikubwa cha upinzani,unakiingiza kwenye serikali,hii haifai. Hizi ni hatua tu za dharura ambazo kwa kweli kwa kiutawala wa demokrasia, hazifai kabisa,” alisema.

Sumaye alisema kinachotakiwa ni kuwa na demokrasia ya kweli na kwamba kama chama kimeshindwa uchaguzi,kipishe ili kuruhusu chama kilichoshinda, kuingia madarakani.
‘‘Kama umeshindwa,maana yake sasa wananchi wameona wamchukue mtu mwingine, wewe unapisha.Kama mfano mseto wa nchi za wenzetu,kama umeshinda, lakini ushindi wako hautoshi kuunda serikali,ndiyo sasa unaita serikali ya mseto,lakini humchukui yule mpinzani wako mkubwa,unachukua chama kingine kidogo,kilichoshinda viti vichache,unaungana nacho ili uwe na uhalali wa kuunda serikali,yule mwingine mkubwa,lazima awe bungeni akiwa mpinzani,” alisema.

Akitolea mfano wa Kenya na Zimbabwe,Sumaye alisema hakuna tena upinzani baada ya vyama vikuu vya upinzani kuunganishwa na vyama vilivyoshinda kwa hila.

‘‘Sasa Kenya kuna upinzani gani,Zimbabwe wakiungana, kutakuwa na upinzani gani?Kama Tsvangirai yuko kwenye serikali,Raila Odinga leo yuko kwenye serikali,sasa Kenya mpinzani ni nani?PNU ilikuwa pamoja na KANU kwa utaratibu fulani fulani,Raila yuko na vyama vingine lundo,kile cha Musyioka kiko serikalini, ndiye‘Vice President,sasa Kenya kuna upinzani gani?” alihoji. Kutokana na hali hiyo,Sumaye alizitahadharisha nchi za Afrika kuwa waangalifu sana katika ziku zijazo.

‘‘Hatuwezi kuiba kura,halafu tunaungana na mpinzani mkuu ndiyo tunajidai tunatatua tatizo, kwa sababu tu sasa wote tunakula,hivi sababu ya kuunda vyama vya upinzani ni kula tu?Naona hapo sasa tunachohangaikia ni kula.Mimi hiyo kabisa naikataa,”alisema.
Alitoa changamoto kuwa kitu ambacho nchi za Afrika zinapaswa kuwa nacho ni kuwa na demokrasia ya kweli.

‘‘Umeshindwa,unampa mwenzako mkono,unaenda kuimarisha chama chako, baada ya miaka mitano, uko ulingoni,si habari ya kung’ang’ania,”alisema.
‘‘Pili,hii habari ya kuchukua chama,kama ni chama tawala,kinachukua chama cha upinzani kikubwa,kuungana nacho mseto,si sahihi,” alisema.

‘‘Kama suala ni kupeana mshahara,mpe kazi nyingine basi.Si lazima hii ya kisiasa.Kwa hiyo kwa kweli huko tunakokwenda siko,”alisisitiza Sumaye.

Sumaye ametoa kauli hiyo huku serikali ikijitahidi kurejesha kwenye mstari mazungumzo ya muafaka kati ya Chama cha Wananchi(CUF)na Chama Cha Mapinduzi(CCM),visiwani Zanzibar yaliyosinzia baada ya CCM kukataa kuunda serikali ya mseto na CUF.Habari hii na Martin Malera

No comments: