Saturday, September 26, 2009

from rwanda with lessons part I
Wiki chache zilizopita niliahidi ku-share na blog hii ya jamii mambo machache niliyoyaona Rwanda. Nilimepata msukumo zaidi kutokana na historia ya Rwanda, kwani mwaka 1994 mauaji ya kimbari yalisababisha mauaji ya watu wengi sana, inakisiwa zaidi ya watu 500,000.
Matokeo ya mauaji ya kimbari yaliongeza chuki zaidi kati ya Wahutu na Watutsi. Katika hali ya kawaida, wengi tungetegemea Rwanda ingesuasua na ingedidimia zaidi. Lakini ukienda Rwanda utaona maendeleo makubwa mno; wafanyakazi kuanza kazi saa moja asubuhi, ujenzi, barabara nzuri nk.
Badala ya kuona na kukaa kimya au kuanza kulalamika nimeonelea ni busara kuandika na kushare huku nikitarajia tutaweza kujifunza kwa majirani, ambao kasi yao wengine wanasema wameshatuacha au watatuacha mbali.Haya ni machache; Uongozi bora, Uthubutu wa Wanyarwanda, Usafi na utii wa Sheria, Nyumbani ni Nyumbani na Mipango miji.
Uongozi bora:
Uongozi bora wa Rais Paul Kagame umechangia kwa kiasi kikubwa sana kuifikisha Rwanda hapa ilipo. Wiki iliyopita Rwanda imetajwa na ripoti ya Benki ya dunia kama nchi iliyoboresha zaidi mazingira ya uwekezaji. Tofauti kubwa na nchi nyingi za kiafrika, Mawaziri wanaendesha magari na tena sio mashangingi kama TZ.
Tulishuhudia Rais Kagame mwenyewe akiendesha gari !. Ikiwa Rais anaonyesha mfano mara nyingi viongozi wengine watafata. Kagame amesimamia utawala bora, ukiwa Rwanda na ukafanya kosa hakuna cha wewe nani, jamaa hawapokei rushwa!. Jarida la TIME lilimtaja Rais Paul Kagame kati ya watu 100 wenye ushawishi duniani. Najua kwa kutambua uwezo wa Kagame, Tony Blair hakusita kuwa mshauri wake binafsi!.
Uthubutu wa Wanyarwanda:
Tukifuata historia Wanyarwanda huzungumza kinyarwanda na kifaransa. Hili sasa limebadilika Wanyarwanda wanazungumza kiingereza na Kiswahili vizuri!. Kwa wale wafuatiliaji wa BBC idhaa ya kiwahili, siku chache zilizopita ilizungumzia uanzishwaji wa ufundishaji wa Kichina kwenye chuo kikuu cha Kigali!.  Tayari wanafunzi wengi wanasoma na wanaongea Kichina, hii ni ishara tosha ya uthubutu wa Wanyarwanda, wanatambua umuhimu wa kujifunza lugha nyingine muhimu. Jambo kuu zaidi ni Warwanda kuyapa kisogo yaliyotokea na kuangalia mbele. Dereva wa texi aliyeniendesha alipoteza wanafamilia wote kwenye mauaji yale, lakini anaangalia mbele.


Usafi na Utii wa sheria:
Jambo la kwanza kugundua ufikapo Rwanda ni usafi wa hali ya juu wa jiji la Kigali. Hairuhusiwi kutupa takataka ovyo bali sehemu maalum zilizotengwa. Kusisitiza suala la usafi kila Jumamosi ya mwisho ya mwenzi ni siku ya usafi kila mtu anashiriki katika kufanya kazi za usafi, hili pamoja na sheria zimefanya tabia ya usafi ijengeke. Sheria za usalama barabarani ni msumeno, kila anaendesha pikipiki ni lazima avae kofia pamoja na abiria. Waendesha pikipiki za kukodi wana namba na mavazi maalum ya kazi, hili linafanya kutambulika kwa rahisi. Usalama wa Rwanda ni jambo jingine ambalo ni thahiri, hapa napata swali lisilo na jibu; polisi huwianisha uhalifu wa silaha na nchi zenye au zilizokuwa na machafuko. Iweje Rwanda iliyotoka kwenye machafuko, iko jiranio zaidi na nchi zenye machafuko hadi leo za Burundi na Congo iwe salama hadi mabenki yanafungwa saa nne usiku!.

From Rwanda with lessons – Part II itafuata.
Mdau IK.

No comments: