Saturday, February 13, 2010

Papic Ajitosa Kuwania umakismo

KOCHA wa Yanga, Kostadin Papic awasilisha rasmi barua ya maombi ya kazi Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kuwania nafasi ya kumrithi Mbrazil Marcio Maximo anayemaliza mkataba wake wa kuifundisha Taifa Stars mwezi Julai.

Papic ambaye aliweka bayana dhamira yake hiyo ya kuwania kuifundisha Taifa Stars pale tu TFF ilipotangaza kuanza mchakato wa kumtafuta kocha mpya, aliwasili katika ofisi za shirikisho hilo majira ya saa 5:30 asubuhi akisindikizwa na katibu mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako.

Akizungumza na Mwananchi mara baada ya kukabidhi barua yake, Papic alisema amefikia uamuzi huo kutokana na kuamini kuwa ana vigezo vyote vinavyomwezesha kuwa kocha wa Taifa Stars.

"Bila shaka niliweka wazi kwamba nitaomba kazi ya kufundisha Taifa Stars na sasa nimeleta rasmi maombi yangu hapa kwa kuwa najiamini kutokana na vigezo vilivyotolewa ninavyo,"alisema Mserbia huyo.

Aliongeza kuwa ameshafanya kazi ya kufundisha soka sehemu mbalimbali akiwa na timu kubwa na kuziletea mafanikio, hivyo hana wasiwasi wa kuimudu vema Taifa Stars.

Akizungumzia mustakabali wake na Yanga ikiwa atakabidhiwa nafasi ya kuifundisha Taita Stars, alisema kwa sasa hakuna tatizo hasa kwa kuwa mkataba wake na Yanga unamalizika mwezi Juni na kuongeza kuwa kama atafanikiwa pia anaweza kuwasaidia kutafuta kocha mwingine ikiwa watapenda.

"Mkataba wangu unamalizika Juni hivyo kwa sasa sioni tatizo na kama nitafanikiwa katika hili ninaweza pia kuwasaidia Yanga kutafuta kocha mwingine kama watapenda," alisema Papic maarufu kama Clinton.

Endapo Papic atafanikiwa kuchukua nafasi ya kuinoa Stars, itakuwa zamu ya Yanga kutoa kocha wao kuifundisha timu hiyo ya taifa kwa kuwa mara nyingi makocha wa Stars pindi wanapomaliza mikataba yao ndipo wanaamua kufundisha klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani na Twiga.

Makocha waliowahi kuifundisha Taifa Stars na baada ya kumaliza mkataba wao kujiunga na Yanga ni pamoja na Rudi Gutadrf mwaka 1982, Joel Bendera (1986) kwa sasa Naibu Waziri wa Habari na Utamaduni akiwa kocha wa Stars aliombwa kuisaidia klabu hiyo kwenye michuano ya Afrika mashariki na kati. Mwaka 1996, Yanga ilifanikiwa kumnasa Sunday Kayuni aliyekuwa kocha msaidizi wa timu ya Tanzania Bara.

No comments: