Tuesday, February 2, 2010

jerry muro apasua jipu pwaaaa!

Sakata la Jerry Muro limeingia sura mpya jioni hii baada ya mtangazaji huyo kutinga katika ofisi za gptz na kupasua jipu mara baada ya Kamanda Selemani Kova kuongea na wanahabari mapema leo. Mengi mazito ameongea. Exclusive interview hii ni kwa hisani ya globalpublisherstz.com

TAARIFA YA AFANDE KOVA JUU YA SAKATA LA JERRY MURO

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema lilimshikilia na kumhoji mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro, baada ya kupata taarifa kutoka kwa mwananchi aliyelalamika kwamba kuna matapeli wamekuwa wakimtisha wakimdai rushwa.
Aidha, limesema halina tatizo lolote na mwandishi huyo kama taarifa zilivyovuma na badala yake linafanya kazi kulingana na sheria na taratibu zake.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari na kumtaja mwananchi huyo kuwa ni Michael Wage, ambaye alikuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, kabla ya kuvuliwa wadhifa huo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na ubadhirifu wa fedha.

Alisema Wage alifika katika kituo Kikuu cha Polisi juzi saa 5 asubuhi na kulitaarifu Jeshi hilo, kwamba kuna watu watatu ambao wanajifanya maofisa wa Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), waandishi wa habari na wanajeshi huku wakitoa vitisho wakitaka wapewe Sh milioni kumi.

Alisema mwananchi huyo alilalamika kwamba watu hao wamekuwa wakimwandama na kumsumbua tangu Januari 28 mwaka huu, wakidai kwamba yeye ni fisadi na ana majumba mengi ya kifahari Morogoro, hivyo walitaka wapewe hongo hiyo ili wasimkamate.

Aidha, Kova alisema mwananchi huyo alidai kwamba watu hao ambao walikuwa na pingu, wamekuwa wakimwambia kwamba asipotoa fedha hizo watamchukulia hatua na kumtangaza katika jamii kwa ufisadi.

“Wage alipokuja kwetu, alisema hatoi fedha na anataka watuhumiwa hao wakamatwe na wakawekeana miadi ya kukutana saa 6 mchana katika hoteli ya City Garden katikati ya Jiji kwa makubaliano kwamba watapeana fedha hizo katika eneo hilo ... polisi walifikiri ni matapeli na tukaenda muda huo,” alisema.
Alisema baada ya kufika katika eneo hilo, lengo likiwa ni kuwakamata matapeli hao, gari namba T 545 BEH aina ya Toyota Cresta, liliingia lakini mwenyewe alikataa kushuka na kumtaka Wage alifuate gari hilo.

“Polisi wangu walipoona gari limekuja na watuhumiwa kukataa kushuka, walilifuata na walipofika walishangaa kumwona Jerry Muro na baada ya Wage kusema huyu ndiye ambaye amekuwa akimsumbua sana, polisi ilibidi wamchukue mpaka kituoni ili kupata maelezo mazuri,” alisema.

Kova alisema mlalamikaji huyo alikuwa akidai kwamba anamfahamu Jerry na amekuwa akimsumbua hata kumfuata nyumbani kwake na kukubaliana wakutane jijini Januari 29 mwaka huu na kutoa vithibitisho mbalimbali kwamba anamfahamu ikiwa ni pamoja na miwani yake aliyokuwa ameiacha ndani ya gari lake.

“Wage aliileza Polisi vithibitisho vilivyopatikana katika gari la Jerry ikiwamo miwani yake aliyoisahau, pia alieleza kwamba Jerry anatembea na bastola na pingu na vyote tulivipata katika gari lake na kumhoji ambapo alikiri kuvimiliki,” alisema.

Alisema pingu zilipatikana kwenye ‘dash board’ huku silaha ikiwa kiunoni na katika uchunguzi wa awali wa maeneo yaliyohusishwa na tukio hilo na uhusiano baina ya watu hao, polisi ilifanya upelelezi na kupata uthibitisho kupitia CCTV.

“Pia napenda mfahamu hakuna suala la Jeshi la Polisi na Muro, isipokuwa kuna mlalamikaji na Polisi na hata kama angekuwa ni askari ametenda kosa kama hilo, angechukuliwa hatua za kisheria … Jeshi la Polisi Kanda Maalum hatuna ugomvi na Muro na ni rafiki yetu sana,” alisema.

Alikiri kutambua umiliki halali wa Muro wa bastola CZ97B namba A6466 na kwa upande wa pingu, Kova alisema ni kinyume cha sheria kutokana na kwamba pingu humilikiwa na Polisi au Magereza pekee.

Pia Kamanda alisema Jeshi hilo limemtaka Muro, kuwasilisha risiti ya pingu hiyo, kutokana na kwamba hakuna sehemu yoyote inapouzwa na sheria haimruhusu mtu yeyote kumiliki labda kampuni na ni kwa kibali maalumu.

“Silaha kama hii ukimwonesha mtu ni lazima ashtuke … hivi hata kama wewe ni mwandishi wa habari za uchunguzi, pingu zinahusiana vipi na utafutaji habari? Hii pingu ukimwonesha mtu tena aliyeumwa na nyoka kama Wage lazima ashtuke,” alisema.

Hata hivyo Kova alisema kuwa kesi hiyo haitaenda mahakamani mpaka ipitie kwa wakili wa serikali na kueleza kwamba Jerry yupo nje kwa dhamana na kuwataka watuhumiwa wengine wawili wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo wajisalimishe.

Muro ameibuka kuwa mtangazaji mahiri kwa mwaka 2009 na kujinyakulia tuzo ya Mwandishi Bora wa Mwaka kupitia vipindi vyake vya Televisheni vya Usiku wa Habari vinavyorushwa katika kituo cha TBC1 na kabla ya kuhamia kituo hicho alikuwa akiendesha kipindi kama hicho katika ITV.

Miongoni mwa mambo aliyokuwa akirusha katika vipindi hivyo ni pamoja na rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa sheria na polisi wamekuwa walengwa wakuu wa vipindi hivyo.

Wakati huo huo, Baraza la Habari Tanzania (MCT) limelitaka Jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi haraka na kumfikisha mahakamani Muro ili haki iweze kutendeka.

Akizungumzia suala la kukamatwa kwa Muro, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema hatua iliyochukuliwa na Polisi dhidi ya Muro yawezekana zikawa ni njama za kumtisha asiendelee na uchunguzi wake wa tuhuma kubwa kubwa.

“Muro ana kashfa zingine kubwa anazifuatilia zinazowahusu vigogo wa Serikali, yawezekana hii ni mbinu ya kutaka kumdhoofisha asiendelee na uchunguzi wake … lakini kama ni kweli aliomba rushwa, basi atakuwa ameidhalilisha taaluma ya habari,” alisema Mukajanga alipozungumza na waandishi wa habari jana.

Hata hivyo, alisema Muro asitumiwe kama kondoo wa kafara na kuwaasa waandishi wa habari kuwa makini katika kazi zao wakati huu hususan mwaka huu wa uchaguzi kwani lolote linaweza kuwatokea.

No comments: