Monday, February 22, 2010

JK: Uhusiano wetu na China ni kwa maslahi yetu wenyewe
Na Mwandishi Maalumu, Turkey
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa msukumo wa sasa wa kuwapo kwa uhusiano wa karibu zaidi kati ya nchi za Afrika na China unatokana na mahitaji halisi na maslahi ya kweli kweli ya Bara la Afrika na wala siyo na itikadi.

“Bara la Afrika linatafuta masoko kwa bidhaa zake. Bara la Afrika linatafuta mitaji na uwekezeji katika chumi zake. Bara la Afrika linatafuta teknolojia kwa ajili ya maendeleo yake. China iko tayari kutoa hayo yote. Sasa nongwa iko wapi?” Rais Kikwete amewauliza waandishi wa habari wa Uturuki.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza , Jumamosi, Februari 20, 2010, na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya Uturuki baada ya kuwa amefungua Mkutano wa Pili wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki kwenye Hoteli ya Grand Cehavir mjini Istanbul.

Kiasi cha wafanyabiashara 55 wa Tanzania wanaandamana na Mheshimiwa Rais Kikwete katika ziara yake ya siku tatu nchini Uturuki ambayo rasmi imemalizika . Mheshimiwa Rais Kikwete anatarajiwa kuondoka Uturuki , Jumapili, Februari 21, 2010, kwenda Jordan kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili.

Rais Kikwete ametoa majibu hayo baada ya kuwa ameulizwa nini hasa nia ya nchi kama China na Uturuki ambazo ghafla zimeonyesha hamu kubwa ya kushirikiana kwa karibu zaidi na kujenga mahusiano makubwa zaidi na Bara la Afrika ambalo kwa miaka mingi limekuwa karibu na nchi za Magharibi, na hasa zile ambazo zilizitawala nchi hizo za Afrika.

Rais Kikwete amesema kuwa hamu ya Bara la Afrika ni kuona maendeleo ya haraka kwa watu wake, na nchi yoyote duniani ambayo iko tayari kusaidia azma hiyo ya Afrika inakaribishwa kwa mikono miwili kufanya shughuli na Bara la Afrika.

“Tunaendesha mahusiano yetu kwa misingi ya ushirikiano (partnership) siyo kwa misingi ya nani alitutawala wakati gani. Hakuna nongwa katika hili,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Watawala wa nchi mbali mbali wamebadilika. Sera za nchi mbali mbali zimebadilika. Lakini mahitaji na maslahi ya Afrika yamebakia pale pale. Mahitaji yetu ni masoko kwa bidhaa zetu, uwekezaji katika chumi zetu, upatikanaji wa teknolojia kwa ajili ya maendeleo yetu na nafasi za kuendeleza uwezo wa Bara la Afrika kwa njia mbali mbali na hasa kupitia elimu.”

Rais Kikwete amesema kuwa Bara la Afrika linayo haki ya kutafuta majawabu ya mahitaji yake kutoka nchi yoyote katika pembe yoyote ya dunia na bila kuwekewa masharti kama zinavyofanya baadhi ya nchi.

Amewakumbusha waandishi hao kauli ya kiongozi wa zamani wa China, Hayati Deng Ziyao Ping, ambaye kuhusu maendeleo na nani wa kushirikiana naye katika kutafuta maendeleo, alipata kusema:

“Sijali paka anayo rangi gani ili mradi awe na uwezo wa kukamata panya.”

Rais Kikwete amesema kuwa wakati mwingine ni jambo la kushangaza kuwa baadhi ya nchi ambazo zimewekeza sana katika uchumi wa China na kuifanya nchi hiyo jambari la uchumi duniani, ndizo zinalalamikia nchi za Afrika kushirikiana na China.

Amesema kuwa ni jambo la ajabu kabisa kuwa nchi hizo hizo ambazo zinapiga kelele kuhusu ukaribu wa nchi za Afrika na China, ndizo hizo hizo ambazo zimeshirikiana kwa karibu sana na nchi hiyo ya China.

“Kama nchi hizi kweli zina wasiwasi kuhusu China kuwa na uhusiano wa karibu na Afrika, kwa nini hazina wasiwasi kwa nchi hiyo kuwa karibu na nchi hizo. Kwa nini iwe sawa kwa China kushirikiana na wakubwa hawa, lakini iwe siyo sawa kwa China kushirikiana na nchi za Afrika?”

No comments: