Saturday, April 5, 2008

Kitimtim TRL makao makuu

Na Raymond Kaminyoge

Zaidi ya abiria 100 wa Shirika la Reli Nchini (TRL) ambao walikata tiketi kwa ajili ya kusafiri na treni, `wamevamia` makao makuu ya ofisi hizo na kumbana Mkurugenzi Mkuu Msaidizi, Bw. Dhananjay Naik wakimshinikiza awape usafiri.

Aidha Bw. Naik alipata wakati mgumu zaidi alipokwenda katika ofisi za kukatia tiketi na kukutana na abiria wengine ambao nao walimzunguka na kutaka awaeleze hatima yao.

``Hapa huondoki tueleze tunasafiri vipi kwenda makwetu, fedha mmechukua, usafiri hatuuoni na wala hamtuelezi chochote, tuwaeleweje?`` Alihoji mmoja wa abiria hao, Bi. Magdalena David.

Mkurugenzi huyo ambaye ni raia wa India, kila alipojaribu kuwaeleza abiria hao aliishia kutukanwa matusi ya nguoni na kila alipojaribu kuchomoka katika kundi hilo la abiria wenye hasira walimzuia asiondoke.

``Tunafanya mipango ya kuwarejeshea fedha zenu,`` alisema mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, abiria hao walisema wanataka TRL ikodi mabasi ili yawapeleke kwa sababu nauli watakazorudishiwa haziwezi kutosha kusafiri kwa barabara.

Wakati hayo yakiendelea abiria wengine walipandisha jazba na kutaka kumpiga mkurugenzi huyo lakini akaokolewa na polisi wa kituo kikuu cha polisi cha mkoa ambao walimsindikiza kwenda ofisini kwake.

Hatua ya abiria kudai usafiri inafuatia wafanyakazi wa TRL kugoma kufanya kazi hadi mwajiri wao atakapowalipa nyongeza za mshahara ambapo wanataka kima cha chini kiwe Sh. 160,000 kwa mwezi badala ya Sh. 87,000.

Mwezi uliopita, baada ya wafanyakazi hao kugoma, Menejimenti ya TRL iliahidi kuwalipa wafanyakazi hao nyongeza hiyo ya mshahara mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini halikufanya hivyo hali iliyoanzisha mgomo mwingine.

Kufuatia mgomo huo, huduma za usafiri za shirika hilo zimesitishwa hadi wafanyakazi hao watakaporejea kazini.

Baadhi ya abiria hao walisema wameishiwa fedha za matumizi hali inayowafanya walale katika stesheni hiyo huku wakiombaomba chakula.

Wakati hayo yakitokea, wafanyakazi wa Shirika hilo walioanza mgomo wao tangu juzi, jana waliingia katika siku ya pili na kusisitiza kuwa hawatafanya kazi hadi kieleweke.

Habari zilizopatikana wakati tukienda mitamboni zinasema, uongozi wa shirika hilo jana ulianza kuwarudishia abiria hao nauli zao.

No comments: