Baada ya kuhusishwa katika mazali kadhaa ya mikataba tata likiwemo lile la kusaini mkataba baina ya Serikali na mwekezaji wa mgodi wa Buzwagi, na lile la Richmond, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Bwana Mustafa Nazir Karamagi sasa hana ujanja, bunge limembana kinoma atoe ushahidi kuhusu maelezo yake.
Bw. Karamagi alikwaa soo hilo, baada ya mbunge mmoja kuibua hoja iliyomgusa moja kwa moja na kujikuta hana ujanja zaidi ya kusimama bungeni, na kujieleza ni kwa namna gani anahusishwa na suala lililokuwa linazungumzwa na mheshimiwa huyo.
Soo lenyewe lilikuwa hivi:
Hoja binafsi kuhusu mkataba mwingine tata baina ya Serikali na Kampuni ya kushughulikia makontena bandarini, TICTS, iliwasilishwa na Mhe. Godfrey Zambi wa jimbo la Mbozi Mashariki. Hoja hiyo ilihusu utendaji usioridhisha wa kampuni ya TICTS.
Bw. Karamagi alipoona kampuni hiyo inapigwa mawe, akasimama bungeni kuitetea. Lakini akaanza kwa kukiri mwenyewe kwamba ana maslahi na TICTS kwa kuwa ni Mwenyekiti wa kampuni hiyo na ana hisa za asilimia 30 .
Bw. Karamagi alijikuta akikabiliwa na upinzani mkali wa hoja za waheshimiwa wengine.
Akajikuta akibanwa zaidi pale aliposema kuwa Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya tatu lilikaa na kuamua kuwa TICTS iongezewe muda wa mkataba, kutoka miaka 10 ambao ulikuwa bado haujaisha hadi miaka 25.
Kufuatia kauli yake hiyo, aliyekuwa mmoja wa mawaziri katika Serikali ya awamu ya tatu, Mhe. Anna Abdallah, akaomba ufafanuzi wa Spika, akitumia kifungu 68 (7) cha kanuni za Bunge na kumtaka Karamagi athibitishe kauli yake kwa vielelezo, kwani wakati huo, yeye (Karamagi) hakuwa Waziri na kwamba maamuzi yoyote ya Baraza la Mawaziri huandaliwa kimaandishi na Katibu wa baraza na kusainiwa.
Ombi hilo lilimfanya Spika kumtaka Mheshimiwa Karamagi kutoa ushahidi ama kufuta kauli yake kuwa uamuzi huo ulitolewa na Baraza la Mawaziri.
Akijibu hilo, Mhe. Karamagi akasema anao ushahidi ambao ulitolewa katika majadiliano ya TICTS na Tume ya Kurekibisha Mashirika ya Umma, PSRC.
Kutokana na kauli hiyo, Spika alimtaka kuwasilisha ushahidi huo kabla ya saa 5:00 leo asubuhi ambapo akishindwa, atachukuliwa hatua kutokana na kulidanganya Bunge.
``Ulete vielelezo vinavyoonyesha uamuzi wa baraza la mawaziri. Kama havipo uondoe kauli yako kwamba uamuzi huo ulifanywa na baraza la mawaziri ... hadi kesho saa 5:00 uwe umewasilisha, kama huna, hatua zitachukuliwa kwa kulidanganya Bunge,`` akasema Mhe. Spika Sitta.
Awali, akiwasilisha hoja hiyo, Mheshimiwa Zambi alilitaarifu Bunge kuwa kulikuwa na barua kutoka Wizara ya Fedha ikitaka TICTS kuongezewa muda na kuwa miaka 25.
Mkataba wa awali uliokuwa udumu kwa muda wa miaka 10, ulisainiwa Mei 5 mwaka 2000 na kutakiwa kuisha mwaka 2010.
Mhe. Zambi akasema katika barua ya Septemba 6 mwaka 2005, aliyekuwa Waziri wa Fedha Bw. Basil Mramba aliandika barua yenye kumbukumbu namba TYC/R/160/32 kwenda kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato, TRA, ili aongeze muda wa mkataba na kufikia miaka 25.
``Napenda kukutaarifu kuwa Mheshimiwa Rais ameiagiza Wizara ya Mawasiliano hususan Mamlaka ya Bandari kutekeleza yafuatayo�,`` akanukuu barua hiyo.
Barua hiyo ambayo ilisomwa mbele ya Bunge, inasema kuwa TICTS waruhusiwe kutumia Berth no 8 na ardhi ya karibu nayo, matumizi ya Ubungo Container Deport kuhifadhi mafuriko ya makontena yanayotokana na kuongezeka kwa ufanisi.
Barua hiyo inamtaka Kamishna kufuatilia utekelezaji huo na kutoa ushirikiano wa makini pale mamlaka yake inapohusika hasa kuhusiana na ukusanyaji mapato, kuondoa msongamano uliopo na kutumia kikamilifu mitambo ya TISCAN.
Pia akasema hakukuwa na dharura yoyote ya kulifanya suala hilo zito na nyeti kwa uchumi wa nchi katika mazingira ambayo Bunge na Mawaziri walikuwa wamekasimu kazi zao kwa makatibu wakuu wa wizara walizokuwa wakiziongoza ikiwa ni pamoja na Mhe. Basil Mramba aliyeandika barua hiyo ya kuagiza kuongezwa kwa mkataba huo.
Bunge liliazimia Serikali isitishe nyongeza ya mkataba na kufanya mapitio ya mkataba wa awali ili vifungu vya mkataba huo ambavyo havina manufaa kwa taifa virekebishwe.
Aidha, Bunge likapitisha maazimio kuwa baada ya muda wa mkataba wa awali wa miaka kumi kwisha, nyongeza yoyote ya mkataba au mkataba mwingine mpya uzingatie sheria ya manunuzi wa umma namba 21, ya mwaka 2004.
No comments:
Post a Comment