2008-04-25 09:32:32
Na Lucy Lyatuu
Wanafunzi 415 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani (UDSM), wanachunguzwa na wakikutwa na makosa, watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutiwa udahili.
Hayo yalisemwa jana na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini.
Alisema idadi kamili ya wanafunzi waliofutiwa udahili chuoni hapo baada ya kuhusika na makosa mbalimbali yaliyosababisha vurugu chuoni hapo ni 62.
Hata hivyo, serikali ya wanafunzi chuoni hapo (DARUSO), imesikitishwa na maamuzi yaliyochukuliwa dhidi ya wenzao na kuahidi kutoa tamko lao leo.
Hali katika Chuo hicho jana ilikuwa shwari baada ya baadhi ya wanafunzi kuanza kuingia madarasani.
Profesa Mukandala, alisema wanafunzi wanaochunguzwa miongoni mwao wapo waliokuwa na udhamini binafsi na wanaotoka nje ya nchi ambao walikuwa hawajalipa ada.
Alisema inawezekana wapo watakaokuwa wamelipa ada na hawakujihusisha na vurugu hizo.
``Kabineti ya chuo itakaa na kupitia mmoja baada ya mwingine na endapo watabainika kuhusika, watapewa adhabu ikiwa ni pamoja na kufutiwa udahili,`` alisema Profesa Mukandala.
Kuhusu waliofukuzwa, alisema wapo wanafunzi 15 waliobainishwa na Tume ya Jaji Emiliana Mushi, ambao wameondolewa chuoni na wataweza kuomba wadahiliwe upya pale tu mahakama itakapowaona kuwa hawana hatia.
Aliongeza kuwa wanafunzi wengine watano ambao walikamatwa na bangi, wamesimamishwa masomo, kuondolewa chuoni na kukabidhiwa kwa polisi ili sheria ichukue mkondo wake.
Profesa Mukandala, aliongeza kuwa, wanafunzi wanne waliodaiwa kuwavamia wenzao waliokuwa darasani, wameondolewa chuoni na udahili wao umefutwa na hawataruhusiwa kurudi chuoni hapo tena.
Aliongeza kuwa wanafunzi wengine 38 waliodaiwa kuanzisha mgomo juzi wakishinikiza wenzao kurudishwa chuoni, nao wamefutiwa udahili wao.
Alisema wanafunzi hao walikamatwa na FFU waliokuwa wakilinda amani chuoni hapo na kupelekwa rumande ambapo Jumatano walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza.
Aidha, aliongeza kuwa Bodi ya Mikopo imeshapewa taarifa za kufutiwa udahili kwa wanafunzi hao ili wasiendeleze utaratibu wa mikopo.
Akitoa maoni yake, Rais wa DARUSO, Bw. Deo Daud, alisema amesikitishwa na maamuzi yaliyotolewa dhidi ya wanafunzi hao na kwamba si kweli kwamba walihusika.
``Katika shika shika ya polisi, wanaweza kuwahusisha waliomo na wasiokuwamo, hivyo mahakama ndio ilitakiwa itoe haki,`` alisema Bw. Daud.
Aliongeza kuwa wanafunzi hao walitakiwa kusikilizwa ili wapewe adhabu inayostahili na matendo yao na sio kuwatisha ili warudi madarasani.
Bw. Daud, alisema maamuzi yaliyotolewa ni ya kibabe, yenye vitisho na ya kisiasa zaidi kwani wanafunzi ambao hawajalipa, hawana uwezo na hivyo si sahihi kuwafukuza.
Naye Mhadhiri Mstaafu, Profesa Issa Shivji, alisema maamuzi ya kuwafukuza wanafunzi chuoni hapo sio suluhu ya matatizo, bali walitakiwa kukaa katika meza ya majadiliano.
Alisema huwezi kuwa na maamuzi ya haraka namna hiyo kwani inaweza kusababisha migawanyiko katika jamii.
No comments:
Post a Comment