Asasi tano zisizokuwa za kiserikali leo zimefungua kesi ya msingi kupinga kanuni zinazodai kuwa batili zilizoko kwenye sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu, kanda ya Dar es Salaam, kupinga kanuni ya 6 na kanuni ya 7 ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995.
Mashirika hayo yanadai kuwa kanuni hizo zina vipengele ambavyo vinaweka vingamizi visivyo vya lazima vya kumzuia mwananchi kuwa na haki ya kupata taarifa zinazotolewa na viongozi wa umma kuhusiana raslimali, mapato au madeni yao.
Mashirika yaliyofungua kesi hiyo ni Mtandao wa Asasi zilizo Kusini mwa Afrika zinazojishughulisha na haki za Binadamu- SAHRINGON, Taasisi ya Vyombo vya habari Kusini mwa Afrika-MISATAN-, Asasi inayojishughulisha na Haki za Wanawake-KIVULINI- na Shirika la Kitaifa la Msaada wa Kisheria-NOLA- na Chama cha Wanahabari Wanawake-TAMWA.
Katika kesi hiyo, taasisi hizo zinaitaka mahakama itamke kanuni hizo walizozianisha katika madai yao ni batili na zinapingana na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na pia zinataka mahakama itamke kuwa raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano ana haki ya kupewa, kuchapisha taarifa kuhusiana na mapato, raslimali na madeni ya viongozi wa umma bila vipingamizi ili mradi atatunza maadili na usalama wa Taifa.
No comments:
Post a Comment