2008-04-05 09:36:47
Na Simon Mhina
Hatimaye marehemu Paul Goliama amezikwa kwa taratibu zote za imani ya dini ya Kikriso baada ya hukumu ya mahakama iliyowapa haki hiyo juzi.
Marehemu Paul Goliama alizikwa jana katika makaburi ya Sinza jijini Dar es Salaam chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Alfred Tibaigana alikuwa miongoni mwao.
Kufuatia ulinzi huo, taratibu za maziko zilifanyika kwa amani na utulivu.
Marehemu hakuweza kuzikwa kwa takriban wiki moja, baada ya kuzuka kwa mgogoro kati ya waumini wa dini za Kiislam na Kikristo ambao kila upande ulikuwa ukidai haki ya kuuzika mwili huo kwa imani ya dini yao.
Ibada ya kuhitimisha maziko hayo, iliongozwa na Makamu wa Mkuu wa Jimbo la Kinondoni la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki, Mchungaji Stephen Mwongola.
Mazishi hayo yalifanyika baada ya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni chini ya hakimu Emilius Mchauru kuamuru kwamba wenye haki ya kuzika mwili wa Goliama ni ndugu zake na akawapiga marufuku Waislam kutojihusisha kwa namna yoyote na maazishi hayo.
Ibada ya mazishi ilianza majira ya saa tano asubuhi katika kanisa la Usharika wa Sinza.
Akihubiri katika ibada hiyo, Mchungaji Mwokola, alisema sakata la kugombea maiti hiyo licha ya kutoa changamoto kwa kanisa na jamii, lakini hasa linatakiwa liwe funzo kwa waumini viruka njia, ambao hawana msimamo na dini zao.
Alisema pamoja na uhuru wa mtu kuabudu dini anayotaka, si vema mtu mzima kuwa kigeugeu na kuhama dini kila wakati, kwani jambo hilo huleta utata kama ilivyotokea.
Hata hivyo, alimsifu marehemu Goliama kwa msimamo wake wa kutubu, uliompa fursa ya kukutana na Kristo.
Kama alivyoahidi mama wa marehemu alipokuwa anazungumza na Nipashe wiki iliyopita, kaburi la marehemu huyo limejengwa kwa zege tupu.
Nia ya kujenga kaburi hilo kwa zege imeelezwa kwamba ni kuepusha uwezekano wa baadhi ya Wislamu hao kumfukua kama walivyokaririwa wakiahidi.
Akizungumza baada ya mazishi, mama wa Marehemu, Bi. Annah Goliama, alisema Waislamu hao wamempa kidonda moyoni ambacho ni vigumu kupona.
``Wamenionea, wamenidhalilisha, sijui kama kuna mzazi mwingine ambaye amefanyiwa haya hapa nchini, yaani kunyang`anywa maiti ya mwanangu kanisani! Sitasahau`` alisema.
Baadhi ya ndugu walisema baada ya kukamilika kwa mazishi hayo watafanya kikao cha familia kuamua hatua zaidi za kuchukua.
No comments:
Post a Comment