Tuesday, January 4, 2011

Mwanasheria Mkongwe na Machachri nchini na Mbunge (Chadema)Mheshimiwa Tundu Lissu
-------------
( Huu ni mchango wangu (maggid mjengwa)wa mawazo kwenye jukwaa la Wanabidii)

Ndugu Yangu, Tundu Lissu na Wengine,
Nauona mjadala huu kuwa ni wa kuelimisha sana. Nimejifunza na naendelea kujifunza mengi kutoka kwa wachangiaji wengine. Nimesoma na kujifunza pia kutokana na fikra yakinifu za ndugu yangu Tundu Lissu juu ya hili la Katiba. Na kwa Tundu Lissu ningemshauri asifanye makosa yale yale yanayofanywa na wengine; mathalan, hatuna sababu za kuitana maCCM, maCHADEMA, maCUF na mengineyo. Mwisho tutaishia kuitana maPinzani, maBedui, nduli na mengineyo. Tutakuwa tumetoka kwenye njia iliyo sahihi ya kuendesha majadiliano haya muhimu kwa taifa letu.

Nakumbuka John McCain kwenye moja ya mikutano yake ya kampeni alimkatisha shabiki wake aliyeanza kutoa kauli za kibaguzi juu ya Obama. McCain akatamka; “ Acha hayo, nataka niwaambie, Barack Obama ni Mmarekani mwenzetu. Ni mtu mwuungwana na anaishi vema na familia yake. Tubaki kwenye hoja za msingi”. Na katika Tanzania yetu wenye fikra za kuipinga CCM na Serikali wamekuwa wakitengwa na hata kupewa majina mabaya. Nimeshawahi kumsikia mtu akiambiwa;

“ Alaa, unaongea na Lipinzani hilo!” Kana kwamba aliyeitwa ‘ Lipinzani’ hakuwa Mtanzania na binadamu kama wengine.

Ndio, kwenye fikra za Tundu Lissu kuna mahali pia nadhani Tundu Lissu hakunielewa vema katika kile nilichoandika. Hapa nitaweka rekodi sawa juu ya tofauti ya alichoandika Tundu Lissu na nilichoandika mimi. Tundu Lissu anaandika, namnukuu;

“Na ukweli wa Mungu ni kwamba alichokisema Kikwete jana juu ya Katiba mpya sio tamko muhimu kuliko yote yaliyopata kutolewa tangu uhuru kama anavyodai kaka Maggid. Na wala sidhani, given skandali zote za utawala wake tangu kuingia kwake madarakani '05, kwamba huyu ni Rais anayestahili sifa zote alizomwagiwa humu ndani. Au pengine mimi nina wivu wa kijinga kama alivyowahi kututukana Mkapa kipindi fulani!”( Tundu Lissu)

Nilichoandika mimi, najinukuu;

”Kwanza kabisa nataka niseme, kuwa hotuba ile ya Rais Kikwete ni ya kihistoria. Ni moja ya hotuba muhimu sana katika historia ya nchi yetu tangu tupate uhuru. Maana, jambo lile la nne na la mwisho lililozungumzwa na Rais wa Awamu ya Nne kwenye hotuba yake, ndilo jambo lililofungua ukurasa mpya wa taifa letu baada ya miaka 50 ya uhuru. “ ( Maggid Mjengwa)

Nimeandika kuweka sawa tu. Sina nia ya kuanzisha mjadala mwingine mpya mbali ya huu muhimu wa Katiba tunaoendelea nao sasa.

Na

Maggid Mjengwa

No comments: