Kocha Azam ageuka gumzo Zanzibar |
Jackson Odoyo, Zanzibar WAKATI pazia la mashindano ya Kombe la Mapinduzi likifunguliwa leo kwenye Uwanja wa Amaani mjini Zanzibar, kocha mkuu wa Azam, Stewart Hall amekuwa gumzo mjini hapa. Kocha huyo amekuwa gumzo mjini hapa kufuatia uamuzi wake wa kuachana na timu ya taifa ya Zanzibar,Zanzibar Heroes na kujiunga timu hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Said Bakhressa. Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti mjini hapa mashabiki wamekuwa na imani na Azam kuwa itafanya vizuri kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata kocha huyo akiwa na Zanzibar Heroes. ìSisi tuna imani na kocha huyu (Hall) kwa sababu ni bora hivi sasa katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa hapa na Zanzibar Heroes, hivyo tuna imani kuwa ataiwezesha Azam kunyakua Kombe la Mapinduzi, îalisema Masoud Suleiman Chile. Chile ambaye alikuwa mchezaji chini ya kocha huyo alisema Hall amefanikiwa katika timu ya taifa na tayari ameshaanza kuonyesha uwezo wake akiwa na Azam, hivyo anaamini kuwa timu hiyo itatisha katika mashindano hayo. Wakati mashabiki wakiwa na imani na timu hiyo, ratiba ya mashindano hayo inaonyesha kuwa Azam itafungua pazia la mashindano hayo kwa kupambana na Chuoni iliyopanda daraja msimu huu kutoka Kundi A. Wakati pambano la Azam na Chuoni litaanza saa 10:30 jioni mechi nyingine itakuwa kati ya timu ya Yanga na Zanzibar Ocean View, ambayo itachezwa saa 2:30 usiku. |
No comments:
Post a Comment