Monday, April 14, 2008

Utajiri wa Chenge waishitua Ikulu

*Ni kuhusu kumiliki akaunti ya Sh 1 bilioni

*Yasema inasubiri taarifa rasmi sheria ichukue mkondo

*Profesa Lipumba kuuzungumzia leo

Ramadhan Semtawa, Dodoma na Muhibu Said, Dar

SIKU moja baada ya Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, kudaiwa kumiliki dola 1 milioni nje ya nchi, serikali imesema sheria itachukua mkondo wake kuona fedha hizo amezipataje.

Hatua hiyo itafanyika baada ya taarifa rasmi kuhusu utajiri wa waziri huyo kufika serikalini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, alisema taarifa rasmi zikifika, sheria itachukua mkondo wake kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria. Simba alisema hata yeye hayuko juu ya sheria.

Waziri Simba aliongeza kwamba, taarifa zikifika itaangaliwa katika kumbukumbu za Chenge katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Umma.

Alisema Chenge kama viongozi wengine, amejaza fomu za kutaja mali zake hivyo kama amedanganya, itajulikana.

Simba alipoulizwa anachukuliaje taarifa za waziri kumiliki fedha nyingi kama dola 1 milioni, alijibu: "Hata mimi nashangaa kama wewe iwapo alizipata kihalali au la."

Alisema hadi sasa taarifa hizo zinafanyiwa kazi nchini Uingereza.

"Ni vema watu wakawa na subira katika jambo hilo. Lakini kuna mtu nimemwambia, labda kauza ng'ombe wao wote ndio akapata hizo pesa, labda watu hatujui, au ana biashara nyingine," alisema Waziri Simba.

Kauli hiyo ya Waziri Simba imetolewa siku moja, baada ya Gazeti la The Guardian linalochapishwa nchini Uingereza, katika toleo lake la juzi, kueleza kuanza kwa uchunguzi dhidi ya Waziri Chenge, kutokana na akaunti yake kukutwa na zaidi ya dola 1 milioni.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, taasisi ya kuchunguza makosa makubwa ya jinai nchini humo, ijulikanayo kwa jina la Serious Fraud Office (SFO), inatarajia kuanza upya kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ili kuangalia iwapo zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa, wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28, ambazo ni sawa na Sh 70 bilioni, mwaka 2002.

Gazeti hilo lilieleza kuwa uchunguzi huo wa SFO unatarajia kuanza katika kipindi cha wiki sita zijazo.

Kwa mujibu wa habari hizo, uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba, moja ya mambo yanayofuatiliwa ni kujua iwapo fedha hizo zinazoaminika kuwa za Waziri Chenge, zilizowekwa katika akaunti moja iliyoko katika Kisiwa cha Jersey, zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutoka katika Kampuni ya BAE System, inayotuhumiwa kuinyonya Tanzania kwa kuiuzia rada hiyo kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa.

The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, liliripoti kuwa taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.

Gazeti hilo lilimkariri Waziri Chenge akikiri kwamba, fedha hizo ni mali yake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika serikali ya awamu ya tatu.

Septemba 15, mwaka jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, walimtaja Waziri Chenge katika orodha ya vigogo 11, wakiwamo viongozi kadhaa wa serikali nchini, wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi wa mabilioni ya shilingi za walipakodi.

Baadaye, Septemba 19, Waziri Chenge aliliambia gazeti hili kuwa, walioibua hoja ya ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali kama wakipata au kama wana ushahidi, yeye binafsi anatoa ruksa waupeleke katika vyombo husika vya dola ili ufanyiwe kazi.

Hata hivyo, Chenge alithibitisha kwamba yeye ni mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Tangold, ambayo inamilikiwa na serikali na kwamba, hakuna kifungu cha sheria kinachomzuia kuwa mkurugenzi.

"Nasubiri nipate hizo tuhuma kwa maandishi maana siwezi kuzungumza tu bila kuziona, lakini kama ni ukurugenzi Tangold, mimi siyo kwamba niliwahi kuwa mkurugenzi, ni mmoja wa wakurugenzi hadi sasa. Hii ni kampuni ya serikali, tatizo nini?" alihoji Chenge na kuongeza:

"Lakini kama mtu ana ushahidi wa tuhuma za ufisadi, jamani tunavyo vyombo vyetu, si wapeleke zikafanyiwe kazi," alisema Chenge.

Waziri huyo alisema hapendi malumbano, isipokuwa yote yaliyozungumzwa atahitaji kuyaona kwa maandishi na uonyeshwe ushahidi wa yeye kuhusika moja kwa moja na ufisadi uliotajwa.

Februari 12, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alitangaza Baraza jipya la Mawaziri baada ya Februari 7, kulivunja baraza la awali ambapo baadhi ya mawaziri na manaibu mawaziri waliachwa na kumteua Chenge kuendelea na wadhifa wake katika Wizara ya Miundombinu.

Hata hivyo, uteuzi wa Chenge kuendelea na wadhifa aliokuwa nao katika wizara hiyo, ulizua mjadala mkali kutoka kwa wananchi, ambao wakidai kuwa hafai kutokana na kuhusika kwake na mikataba mibovu akiwa Mwanasheria Mkuu katika serikali ya awamu ya pili na ya tatu.

Pia baadhi ya wananchi walisema tangu ashike wadhifa huo mwaka 2005, hakuna mabadiliko katika ujenzi wa barabara zaidi ya mafanikio na ufanisi vilivyoachwa na serikali ya awamu ya tatu, ambayo John Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi.

Pamoja na malalamiko hayo ya wananchi, Waziri Chenge aliwaambia waandishi wa habari kuwa, hawezi kujiuzulu kutokana na maneno ya watu na kwamba, suala la yeye kuendelea kukaa katika baraza hilo aulizwe Rais Kikwete ambaye ndiye aliyemteua.

Chenge alisema hayo mara tu baada ya kuapishwa na Rais Kikwete kuendelea kuiongoza wizara hiyo katika sherehe za kuwaapisha mawaziri katika Ikulu ya Chamwino, mjini Dodoma Februari 13, mwaka huu.

Akizungumzia taarifa hizo, Dk Slaa alisema ni habari za kutisha kwani mshahara na posho zake haziwezi kumfanya kuwa na akiba kubwa kiasi hicho.

"Huyu Waziri wa Tanzania ambaye mshahara wake tunaujua, posho zake zinajulikana lazima aeleze alipata wapi fedha hizo," alisema.

Dk Slaa alisema SFO wanafanya uchunguzi wa kwao na kwamba Chenge ni shahidi tu.

"Nilishamuomba Rais Kikwete amwondoe uwaziri na uchunguzi wa kina ufanyike, yatagundulika ya ajabu," alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, leo atakutana na waandishi wa habari, ambapo pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kuzungumzia tuhuma hizo za umiliki wa fedha nyingi dhidi ya Chenge.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma wa CUF Zanzibar, Salim Bimani, aliliambia gazeti hili jana kuwa, Profesa Lipumba atakutana na waandishi wa habari, kuzungumzia suala hilo katika makao makuu ya chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam wakati wa asubuhi.

"(leo) saa 5:00 Profesa (Lipumba) atakuwa na press conference (mkutano na waandishi wa habari) makao makuu Buguruni, kuzungumzia hilo suala la (Waziri) Chenge," alisema Bimani, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa.

No comments: