
Elizabeth Suleyman na Joymertha Ishengoma
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kivukoni, jijini Dar es Salaam, imeamuru mwili wa marehemu Paul Goliama (41) uliokuwa ukigombewa na waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo, uzikwe na ndugu zake kwa dini yao ya Kikristo.
Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Emillius Mchauru baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa walalamikaji (Wakristo).
Akisoma hukumu hiyo juzi, Hakimu Mchauru alisema upande wa utetezi (Waislamu) umeshidnwa kutoa ushahidi wa kuiridhisha mahakama kuhusiana na mgogoro husika, jambo ambalo limemfanya afikie uamuzi huo.
Hakimu huyo alisema wakati Imamu wa Msikiti wa Swafwa, Othman Njama akidai kuwa alimfahamu marehemu tangu mwaka 1998 alipoanza rasmi kuswali katika msikiti wao, baada ya kumwoa binti wa Kiislamu, kwa ushahidi ndugu zake wameiambia mahakama kuwa alikuwa kanisani tangu kuzaliwa kwake na kwamba hajawahi kuwaeleza kuwa amebadili dini.
Alisema wosia unaodaiwa na Waislamu kuwa umeandikwa na marehemu, sio wa kuaminika kwani wosia huo haukuandikwa kwa ushahidi wa aina yoyote ile.
Alisema mbali na hilo, wosia huo una mapungufu mengi, ikiwa ni pamoja na jina la marehemu kuwa la Kikristo wakati Waislamu wamedai kuwa wakati huo alishasilimishwa na kuitwa Shaibu Goliama.
"Kwa nini marehemu aandike wosia kwa usiri na kuupeleka kwa Imamu na sio kwa ndugu, vyombo vya dola au sehemu yake ya kazi?," alihoji Hakimu Mchauru.
Alisema pia kuwa mahakama imetoa haki kwa ndugu wa marehemu kwa sababu, kabla ya kufariki kwake amedaiwa kuacha wosia kwamba binti yake aliyezaa na mwanamke wa Kiislamu atambulike kama Muislamu, kauli ambayo mama mzazi wa marehemu alisema kuwa tangu kuzaliwa kwake binti huyo alikuwa akitumia jina la Kikristo.
Upande wa madai katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2008, ulioongozwa na Wakili Mutakyahwa Charles wakati upande wa wadaiwa ulikuwa unaongozwa na Wakili Aboubakar Salim.
Wadai katika kesi hiyo, ni mama mzazi wa marehemu, Anna Goliama pamoja na mke wa marehemu, Agnes Goliama na mdaiwa ni Imamu wa Msikiti wa Swafwa, Othman Njama.
Katika ushahidi wake, upande wa madai ulidai kuwa marehemu enzi za uhai wake, alikuwa ni Mkristo na kwamba, hakuwahi kuieleza familia yake kuwa alibadili dini na kuwa Muislamu na kuwasilisha vielelezo sita kama ushahidi wao mahakamani.
Vielelezo vilivyotolewa mahakamani hapo na wadai, ni pamoja na cheti cha ubatizo wa marehemu, talaka ambayo marehemu aliitoa kwa mke wa kwanza Attala, barua ya uthibitisho kutoka kanisani inayoonyesha kuwa marehemu Paul alitubu na kurudishwa kundini.
Vielelezo vingine vilivyotolewa, ni nakala za kadi ya NSSF, kadi ya benki, kitambulisho cha mfanyakazi, nakala ya barua ambayo ilitolewa na Waislamu siku ambayo waliwavamia kanisani wakienda kuuzika mwili na kitabu cha kanisa kinachoonyesha kuwa, marehemu alirudi kanisani kutubu na kupewa namba 91.
Kwa upande wa wadaiwa, shahidi ambaye ni Imamu wa Msikiti wa Swafwa, Njama alidai kuwa marehemu alikuwa muumini wake na kwamba, alikuwa akimfahamu kwa jina la Swahib Paul Goliama.
Alidai mwaka 2004, marehemu alimpelekea barua na kumwambia kuwa, barua hiyo iwe kithibitisho pindi atakapokufa na kuwa alikuwa ikieleza kuwa atakapokufa azikwe Kiislamu.
Marehemu Goliama, alifariki dunia Machi 25, mwaka huu na baada ya taratibu zote za mazishi kukamilika wakati ndugu wa marehemu wakiwa kanisani kwa ajili ya kuuombea mwili huo tayari kwa kwenda kuzika, ghafla walitokea waumini wa Kiislamu wakiongozwa na Imamu wao na kudai kuwa alikuwa Muislamu na hivyo kuwazuia kuutoa mwili huo.
No comments:
Post a Comment