*Zoezi kuanza Jumanne Makao Makuu Polisi
*IGP, Gavana Ndulu kusimamia zoezi hilo
*Lengo ni kupunguza makali ya maisha
Ramadhan Semtawa na Tausi Mbowe
WAKATI miezi sita ikiwa haijakamilika, mafisadi waliochota mamilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo wanaanza kumwaga mapesa hayo kwa Watanzania.
Uamuzi huo umekuja baada ya serikali kuwabana mafisadi hao walipe fedha hizo ili zitumike kupunguza makali ya maisha kwa Watanzania waliowengi, ambao wamekuwa wakipata mlo mmoja kwa siku.
Hadi jana fedha zilizorudishwa na mafisadi, zilivuka lengo kutoka Sh 133 bilioni mabazo ziliibwa katika EPA hadi kufikia Sh200bilioni ambazo ni ongezeko la Sh67bilioni.
Kutokana unyeti wa zoezi hilo, Jeshi la Polisi Makao Makuu ambako malipo hayo yatafanyika limeandaa ulinzi mkali ikiwemo wa mbwa kuhakikisha hakuna mtu anavuruga zoezi la malipo hayo ya mabilioni kwa kila Mtanzania.
"Tumeamua kuweka ulinzi mkali, askari wetu wamejiandaa vya kutosha kuweza kukabaliana na vurugu za aina yoyote wakati wa malipo ya fedha hizo," alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Said Mwema, wakati akizungumzia zoezi hilo.
IGP Mwema alifafanua taratibu za watakaoweza kupata mgawo huo kwamba, wote ambao ni Watanzania wa kuzaliwa, ambao wanapaswa kuwa na vyeti halisi vya kuzaliwa, kitambulisho cha kupigia kura au hati ya kusafiria.
Akizungumzia mchakato huo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, alisema uamuzi huo unatokana na kuona makusanyo yamezidi lengo lililowekwa.
Profesa Ndulu alifafanua kwamba, kutokana na makusanyo hayo kuzidi lengo uongozi wa BoT uliishauri serikali kugawa ongezeko kwa wananchi wenye maisha magumu ili kutimiza ahadi ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.
"Tumeona ni vema ongezeko tuligawe kwa Watanzania ambao wamekuwa wakipata mlo mmoja kwa siku, hii pia ni sehemu ya kutimiza ahadi ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania,"alisistiza Profesa Ndulu.
Hata hivyo, alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kuchunguza Mafisadi wa EPA, Johnson Mwanyika ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema orodha kamili ya mafisadi itatangazwa baadaye kwa sasa zoezi linalofanyika ni kugawa mabilioni kwa Watanzania.
"Jambo la muhimu kwanza lilikuwa kukusanya pesa, kinachofuata ni kuzigawa kwa Watanzania, hatua ya kutangaza majina kamili ya mafisadi hao ikiwa ni pamoja na kuwafungulia mashitaka, itafuata baada ya kukamilika mchakato," alisisitiza Mwanyika.
Hata hivyo, IGP Mwema, Profesa Ndulu na Mwanyika wote kwa pamoja hawakueleza zoezi lingeanza saa ngapi na kukamilika kwa muda gani.
Badala yake, walisema taarifa zaidi zitatolewa leo katika taarifa yao mpya kwa umma kupitia vyombo vya habari.
Aprili Mosi, siku ambayo ni maarufu Duniani kama Sherehe ya Siku ya Wajinga.
No comments:
Post a Comment