Wednesday, April 16, 2008

chenge atua bongo kujibu mapigo


Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge akijibu mwasali ya waandishi wa habari juu ya shutma za kujilimbikizia fedha muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam jana mchana akitokea nchini China katika alikokuwa ziarani na Rais jakaya Kikwete.picha kwa hisani ya Mroky Mroky


Takwimu utajiri wa Chenge zaanikwa

WAKATI wasomi na wanasiasa wakizidi kukuna vichwa kuhusiana na taarifa kwamba akaunti ya nje ya Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, imekutwa na akiba ya sh. bilioni mmoja, mchumi mmoja jijini Dar es Salaam amefanya hesabu zisizo rasmi na kubaini kuwa kwa kipindi cha utumishi wake serikalini, waziri huyo ni jambo gumu kukusanya utajiri huo.

Mchumi huyo alisema fedha hizo zinazodaiwa kuwepo kwenye akaunti yake zinatosha kumwezesha Bw. Chenge kuingia kwenye orodha ya watu wachache nchini wanaomiliki fedha nyingi bila kuwa wafanyabiashara.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu Dar es Salaam jana, mchumi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha siasa cha TPP-Maendeleo, Bw. Peter Mziray, alisema amefanyakazi serikalini, hivyo anafahamu kipato cha watumishi wa Serikali ndio maana anatilia shaka utajiri wa Bw. Chenge.

Mchumi huyo alianza kuchambua kipato cha Bw. Chenge kuanzia mwaka 1991 katika makisio ya takwimu zisizo rasmi akisema kuwa kama kila mwezi alikuwa akijiwekea akiba ya dola 2,000 hadi kufikia mwaka 1995 angestahili kuwa na akiba ya dola 12,000.

Hata hivyo alisema kipato hicho bado kingekuwa kikubwa kutokana na hali ya maisha ya Watanzania na matumizi yalivyo.

Alisema alipoteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni wazi kipato chake kilitegemea mshahara, semina na safari ambazo si nyingi kama ilivyo kwa wanasiasa.

Alisema kwa kuwa Mwanasheria Mkuu ni mbunge kutokana na wadhifa wake na kama alikaa bungeni kwa miaka kumi angeweza kupata dola 9,230 sawa na sh. milioni 120 za kitanzania kwa thamani ya dola moja kwa sh. 1,300.

Bw. Mziray alisema inabidi Watanzania wawe makini wafahamu sio kosa kwa mtu kuwa na fedha nje, lakini hoja ya msingi ni jinsi alivyozipata sh. bilioni 1 kwani alisema kwa mtumishi wa umma ambaye wananchi wanajua kazi zake za kila siku ni vigumu kukusanya utajiri huo.

Bw. Mziray alisema asigeweza kushangaa kama Bw. Chenge angekuwa na akiba ya dola 50,000 hadi 100,000 lakini zaidi ya hapo ni lazima Watanzania waanze kuhoji alizipataje.

Alisema ili kujua ukweli, Bw. Chenge alipataje kiasi hicho cha fedha inabidi kuangalia mtiririko mzima ulivyokuwa ili kujua ziliingia kipindi gani, kutoka wapi na akina nani walikuwa wakiziweka katika akaunti yake.

Alisema kama ziliingia katika kipindi ambacho alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kipindi hicho ndicho kiliingiza Taifa kwenye mikataba mibovu watu wanastahili kuzihusisha na mikataba hiyo.

Alisema kuna haja ya Bw. Chenge kuhojiwa ili aeleze alizipata vipi. "Kama angekuwa mfanyabiashara hizi si hela nyingi," alisema Bw. Mziray na kuongeza fedha hizo si rahisi akawa nazo mfanyabiashara wa daladala, kuku au ng'ombe.

Alisema ikiwa ataonekana alijipatia kipato hicho kwa njia zisizo sahihi basi inabidi ieleweke kwamba hiyo ni shutuma nzito kwa mwanasiasa na kujiuzulu kwake hakutoshi.

Alisema kinachotakiwa na Serikali kuona umuhimu wa kuanzisha kitengo cha kuchunguza mafisadi kwani Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) haiwezi.

"TAKUKURU haina ubavu huo, haiwezi kuchunguza rushwa ya ngono kisha itoke huko iende kuchunguza mafisadi," alisema Bw. Mziray. Alisema kwa sasa ni wakati wa Rais Kikwete kupima mwenyewe jinsi ya kuwaeleza Watanzania mwaka 2010 vinginevyo atapata shida sana wakati wa uchaguzi. Habari kwa hisani ya majira.co.tz

No comments: