Mramba ruksa kuhudhuria vikao vya Bunge
Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, ameruhusiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kuhudhuria Mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu. Hata hivyo, mahakama hiyo imesema inaweza kumwita wakati wowote itakapomhitaji kwa sababu mbalimbali zinazoweza kujitokeza. Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Hezron Mwankenja, alisema jana kuwa ametoa uamuzi huo baada ya kusoma vifungu mbalimbali vya Katiba na kuona hakuna sababu ya kumzuia. ``Lakini tufahamu kuwa ruhusa hii, haizuii mahakama kumwita wakati wowote itakapomhitaji hata kabla ya tarehe ya kusikiliza kesi yake ambayo ni Februari 2 mwaka huu,`` alisema. Alisema Ibara ya 17 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatoa fursa ya uhuru wa mwananchi kutoka sehemu moja ya nchi kwenda nyingine. Vilevile, Mwankenja alisema Ibara ya 13 (6) (b) (Presumption of Innocense), inasema mahakama pekee ndiyo yenye uwezo wa kumtia hatiani mshtakiwa hivyo kumyima ruhusa ya kusafiri ni sawa na kumhukumu kabla hajatiwa hatiani na mahakama. ``Justice must be done and seen to be done`` alisema Mwankenja akimaanisha kuwa haki lazima itendeke na ionekane dhahiri kuwa imetendeka. Hata hivyo, Mwankenja alisema Sheria za Bunge hazijaweka wazi kuhusu utaratibu mbunge anapopatwa na matatizo kama ya Mramba. Hakimu alisema Dodoma ni karibu hivyo ni rahisi kwa mshtakiwa huyo kusafiri mara moja na kufika Dar es Salaam endapo atahitajika, hivyo hakuna sababu yoyote ya kumzuia kusafiri. Alisema wadhamini wake lazima waarifiwe kuhusu ruhusa hiyo ya kusafiri ili wasiwe na hofu. Kesi ya Mramba na mwenzake Daniel Yona itatajwa tena tarehe 2 mwezi ujao. Mramba aliwasilisha ombi hilo kupitia wakili wake Herbert Nyange Januari 2 mwaka huu akitaka ruhusu ya kwenda jimboni kwake. Barua ya ombi hilo ilielekezwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo ikitaka ruhusa ya kuwa nje ya Jiji la Dar es Salaaam kuanzia Januari 3 mwaka huu hadi mwezi ujao. Mramba na Yona wanakabiliwa na makosa ya kutumia madaraka yao vibaya kwa kuipatia mkataba wa kukagua uzalishaji wa dhahabu kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza na kampuni yake tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation, kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2002 na ile ya Madini ya mwaka 2002. Katika shitaka la pili, Mramba na Yona wanadaiwa kuwa Mei 28, mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma jijini Dar es Salaam, wakiitumikia serikali katika nafasi za uwaziri wa Fedha na Nishati na Madini, kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mikataba ya kuiongezea kampuni hiyo muda wa miaka miwili wa kuendelea kukagua madini ya dhahabu kuanzia Juni 2005 hadi Juni 2007 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
SOURCE: Nipashe
SOURCE: Nipashe
No comments:
Post a Comment