Thursday, June 26, 2008

Wakazi wa Sinza walia na ongezeko la vibaka, wezi
Na Francisca Jeremiah na Abdul Mitumba, Sinza

Watu wanaodaiwa kuwa ni wezi maarufu kama vibaka, wameendelea kuitikisa kata ya Sinza na vitongoji vyake kwa kukata nyavu za madirisha kisha kuiba fedha, nguo na vitu vingine vya thamani nyakati za usiku.

Vibaka hao pia wanadaiwa kuvizia na kuvamia watu wanaoamka asubuhi na mapema kwa mapanga na nondo kisha kuwajeruhi kabla ya kuwapora fedha, simu na wakati mwingine kadi za magari.

Hali hiyo imesababisha wakazi wa Sinza kuishi kwa mashaka kila siku, hivyo kuomba ofisi ya Mkuu wa wilaya ikishirikiana na ile ya tarafa, kata na serikali za mitaa kuchukua hatua za dharura kukabiriana na hali hiyo ili kuwarejeshea wakazi hao amani.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa hadhara mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Fabian Massawe, walisema kati ya watu kumi waliotoa maoni yao, saba kati walizungumzia kwa kina kuwepo kwa hali hiyo na kueleza wasiwasi wa kutokea machafuko kati ya raia wema na vibaka wasipodhibitiwa.

Mmoja wa wakazi hao, Bw. David Majebele alimwambia DC Massawe kuwa, siku mbili kabla ya mkutano huo, nyumbani kwake pamoja na nyumba ya jirani yake vibaka walikata nyavu za madirisha na kupora vitu vya thamani pamoja na fedha nyingi zikiwemo za kigeni.

Mkazi mwingine aliyetoa dukuduku lake ni Bw. Ray Zumba Alloyce, ambaye alisema matukio mengi mabaya kwa raia yanachomoza kutokana na baadhi ya watendaji wa mitaa ya kata hiyo kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Mkazi mwingine ni wa Sinza E aliyejitambulisha kwa jina la Elizabeth, ambaye amesema hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la vibaka na hivyo kuwafanya waishi kwa mashaka na wasiwasi wa kuibiwa mali zao na hata kudhuriwa.

``Sinza yetu tunalizwa mali kila kukicha, hatuna raha kabisa. Tena vibaka wengine wanafahamaika kwa sababu ni watoto wa majirani zetu... wengine wanatoka mbali, sasa hali imekuwa ni ya hatari, hivyo tungeomba hali hii idhibitiwe,`` akasema.

Akizungumzia suala hilo, diwani mmojawapo wa kata ya Sinza, Bw. Salum Mwaking\'inda, amemueleza DC Massawe kuwa tatizo kubwa walilonalo wakazi wa kata yake ni kupuuza ulinzi shirikishi na kwamba hata michango ya kuwalipa walinzi hawatoi, hali inayokwamisha kuboresha usalama katika kata hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, DC Massawe alishtushwa kusikia kuwepo kwa matukio hayo eneo la Sinza ambalo kwa muda mrefu limekuwa likisifika kukaliwa na watu wastaarabu na wanaopenda kujituma katika kazi halali.

Hata hivyo, Kanali Massawe aliwaagiza watendaji wa mitaa yote mitano ya kata hiyo kusimamia mpango wa Ulinzi Shirikishi Jamii kama moja kati ya njia rahisi kwao kukabiliana na matatizo waliyonayo sasa.

``Kwa kawaida wezi wa aina hiyo huwa wanatoka katika maeneo husika, inawezekana ni watoto wetu au ndugu zetu, hivyo kuwepo kwa ulinzi huo unawashirikisha wananchi wa maeneo husika, bila shaka wizi huo utakoma mara moja,`` alisema.

Mbali na suala hilo la ulinzi na usalama, pia Bw. Masawe aliwataka wakazi wa Sinza kuacha tabia ya kutiririsha maji machafu na pia kutupa taka hovyo katika mitaa yao kwani wanaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa.

No comments: