Thursday, July 31, 2008

Mwiguni George aliyefika katika eneo na kumsaidia Chacha na wenzake!
Mkazi wa eneo la Pandambili, Mwiguni George aliyefika katika eneo la tukio dakika chache baada ya ajali akieleza hali ilivyokuwa. Wanaosikiliza ni ni Kamanda Peter Kivuyo(pili kulia), Kamanda wa Usalama Barabarani wa Mkoa Vitus Nikata ( wa pili tatu kushoto) na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kongwa Ramadhan Kalowa (wa pili kushoto).
Deus Francis Mallya aliyetoa maelezo yenye utata na sasa watu wanamgeuzia kuwa kuna jambo analificha!

STORI MPYA KIFO CHA WANGWE

Utata umejitokezo iwapo marehemu Mbunge Chacha Wangwe aliyefariki katika ajali ya gari Jumatatu usiku alikuwa akiendesha gari hilo ama la.
Kwa mujibu wa mtu aliyefika katika eneo la tukio dakika chache baada ya ajali hiyo, Mwiguni George alimkuta marehemu Wangwe akiwa katika kiti cha mbele cha abiria huku sehemu ya kichwa chaki kikiwa kimebanwa ubavuni mwa kiti hicho na mlango wa nyuma.
Akizungumza Jumanne mbele ya Peter Kivuyo, Kamanda wa Usalama Barabarani wa Mkoa Vitus Nikata na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kongwa Ramadhan Kalowa, mtu huyo alieleza kwamba alikuta mwili wa marehemu Wangwe ukiwa umebanwa ubavuni mwa kiti na mlango wa nyuma huku mkanda wa usalama katika gari ukiwa bado upo mwilini mwake.
“Nilikuwa nyumbani nasikiliza kipindi cha michezo, mida ya saa mbili na nusu usiku hizi, nikasikia kishindo kikubwa, nikakimbilia eneo la ajali. Nilipofika katika eneo la ajali nilimkuta kijana mmoja akiwa analizunguka gari huku akipiga kelele za kuomba msaada,” alieleza Bw. George.
Hata hivyo, mtu huyo alieleza mashaka yake kuwa kulikuwa na watu watatu katika gari hilo na sivyo wawili kamba mabavyo ilitangazwa katika vyombo vya habari.
Deus Francis Mallya alikaririwa mara mwili wa marehemu ulipofikishwa katika hospitali ya Mkoa ya Dodoma akisema kwamba walikuwapo wawili katika safari hiyo na kwamba marehemu Wangwe ndiye aliyekuwa akiendesha gari.
“Nilisikia katika taarifa ya habari kuwa walikuwa wawili. Marehemu ndiye aliyekuwa akiendesha gari na mmoja ndiyo amepona. Mimi ninamashaka, kwani nahisi kuwa na mtu wa tatu na kwamba marehemu hakuwa anaendesha gari wakati wa tukio,” alisema George.
“Nilipofika katika eneo la ajali kulikuwa na mtu mwingine ambaye alikuwa akiwatawanya watu walioanza kufika kwa ajili ya kutoa msaada wasilikaribie gari. Hata hivyo tulianza kuutoa mwili wa marehemu uliokuwa katika kiti cha abiria upande wa mbele,” alieleza George.
“Nilimvua mkanda wa usalama katika kari ambao bado ulikuwapo mwilini mwake, kisha tukamtoa kupitia mlango wa dereva kwani mlango upande aliokuwa amekaa haukuweza kufunguka,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Goerge, hata hivyo, mtu huyo wa tatu alielekeza kutolewa kwa fedha alizokuwa nazo marehemu ndani ya mfuko wa koti, jambo ambalo lilimfanya shuhuda huyo kuhisi kuwa alikuwa pamoja nao.
“Tulianza kutoa vitu vya marehemu, na mtu huyo alielekeza kuwa kuna fedha ndani ya mfuko wa koti,” alieleza na kuhoji kuwa “Sasa mie nikajiuliza kama hakuwa nao alijuaje kuwa marehemu aliweka fedha ndani ya mfuko wa koti,”?
Hata hivyo shuhuda huyo alieleza kuwa wakati pilikapilika zilipokuwa zikiendelea, hakuweza tena kumuona mtu huyo wa tatu, ambaye alitoweka.
Maelezo hayo ya Bw. George yalipelekea Kamanda Kivuyo kuagiza askari waliokuwapo katika eneo hilo kuchukua maeleo ya shuhuda huyo kwa ukamilifu.
“Kwanza nakupongeza sana kwa ujasiri wako, na moyo wa kizalendo wa kutoa msaada kwa marehemu,” Kamanda Kivuyo alimweleza shuhuda huyo.
Maelezo hayo yanaleta mkanganyiko kutokana na taarifa za awali kuwa marehemu Wangwe alikuwa akiendesha gari na kwamba walikuwapo watu wawili katika gari hilo.

No comments: