Thursday, May 6, 2010

MAISHA YA WAWILI (NDOA)
Ieleweke hii nimeipata mahali naomba nioshee na wadau wote wa haka kablog kangu twende kazi !!!
HIVI karibuni nilitembelea mikoa ya Mwanza, baadaye Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine nilikutana na baadhi ya watu na kuzungumza kuhusu mambo tofauti yakiwemo ya ndoa.

Karibu watu wengi niliokutana nao walizungumzia kero katika ndoa huku baadhi yao wakiomba kujua mbinu za kuachana kutokana na kile walichosema kwamba ndoa zimekuwa ni za shida, badala ya faraja waliyoitarajia wakati wanaingia.

Kaka, mimi ni muumini wako, nimekuwa nikisoma sana vitabu na makala ambazo umekuwa ukiandika kwenye magazeti, niliposikia unakuja, nikaona nije nikuone, alisema mama mmoja ambaye aliomba uandikwe mkasa tu, si jina lake.
Nisaidie la kufanya ili niachane na mume wangu maana sioni faida ya kuwa naye.
Swali:Ulitarajia faida gani wakati unaingia kwenye ndoa?
Jibu: Nipate mtu ambaye naweza kusaidiana naye katika maisha,sasa amekuwa ni kero, mambo mengi anajifanyia, kwa mfano sina kazi, yeye ameajiriwa na pia ana biashara, sijui hata huo mshahara wala chochote kuhusu biashara yake, niko tu nyumbani, maisha yangu siyaelewi yanakoelekea.

Swali: Kwa hiyo kuachana ni tiba?
Jibu:Eeeh, bora nijue moja kwamba sina mtu.
Kuna watu wengi ambao matarajio yao kwenye ndoa yamekwenda tofauti. Tafiti zinaonyesha kuwa hali imekuwa mbaya zaidi siku hizi, idadi ya ndoa inaongezeka.
Huenda wewe ukawa ni mojawapo wa waathirika wa matarajio ya ndoa, ulitarajia mazuri, sasa mambo unaona yanakwenda mrama. Fahamu kuwa wewe si mtu wa kwanza.

Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya ndoa hazina amani au matarajio yaliyokusudiwa. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa chuo kikuu cha Loveology kilichoko eneo la West Hollywood, California, Marekani hakuna ndoa ambayo haina mikwaruzo.

Tofauti iliyoko ni akili za watu waliomo kwenye ndoa, kwamba wengine wanapokuwa na mikwaruzo wanaimaliza mara moja wakati wengine wanaikuza.

Mtafiti maarufu katika masuala ya uhusiano Dk D.Ava, ambaye ni kati ya wakufunzi wa uhusiano anasisitiza kuwa jambo la msingi kwa wanandoa ni kufahamu kuwa mikwaruzo ipo na kinachohitajika ni kwa wanandoa wenyewe kuwa na kawaida ya kukaa pamoja kuondoa tofauti zao.

Aidha utafiti mwingine wa chuo kikuu cha Curtin cha Australia, unaeleza kuwa siri ya wanandoa kuwa na maisha bora, kwanza kujuana kwa kina kabla ya kuanza uhusiano.

Tofauti na ilivyokuwa miaka mingi ya nyuma kwamba watu walikuwa wakijuana kabla ya kuanzisha uhusiano, siku hizi wengi wanakurupuka, na hicho ndicho kinachosababisha ndoa nyingi kuvunjika.

Inasikitisha sana kuona watu waliooana tena wengine kwa harusi za kifahari sana, ndoa zao hazina matunda wala kudumu. Kiapo kile walichokula pale mbele ya Watumishi wa Mungu kwamba tutapendana katika raha na shida kinakuwa batili, leo wala hakikumbukwi tena na badala yake kunatokea vitu vinavyoitwa nyumba ndogo na kubwa.

Kwa Wakristo ambao kimsingi kwao hakuna talaka, baadhi ya wanaume wamekuwa wakihama nyumbani na kuhamia nyumba ndogo au wanafanya siri na wengine wanalala pamoja hakuna tendo la ndoa wala kusemezana. Wengine tendo la ndoa wanapata baada ya kutumia nguvu, maana mwenzake hana hamu naye hata kidogo.

Matajiri, wenye vyeo, wasomi n.k nyumba zao zinatisha. Wengi wao wanaigiza tu kuwa wanapendana lakini hakuna ndoa. Sasa tufanyeje ili kuziponya familia hizi zinazosambaratika.

Inawezekana wewe au mimi ni mmoja wa wenye tatizo hili tufanyeje? Kuna baba mmoja ambaye ameoa lakini akawa ana msichana amempangishia na kumhudumia kwa kila kitu, kanisani ni mzee wa usharika kwa sababu ni tajiri, je wewe kama mwenye kuona hali hii unafanya nini?

Ni watu wangapi wanaimba kwaya leo wanafanya huduma mbalimbali kanisani na hata misikitini lakini nyumbani hakukaliki? Tunawasaidiaje watu wa aina hii au tunaishia kusema chini-chini tu basi? Tafakari chukua hatua.

MUHIMU KUZINGATIA:
*Ni muhimu kwa wanandoa kuepuka mazoea, yaani wawe wabunifu, kwa mfano wanaweza wakawa wanapeana zawadi za kushtukiza, au wanaandaliana safari za kushtukiza, hii inamfanya mwenzi wako aone kwamba unamkumbuka.

*Ni muhimu kuwa muwazi. *Mme/mke amsaidie mwenzake kutimiza malengo yake *Utayari wa kusamehe ni jambo jingine muhimu katika kuimarisha ndoa

*Usikumbushie makosa yaliyopita, lakini zaidi ya yote ukikosea kubali na kuwa tayari kuomba msamaha. *Usilale kabla hujamaliza kulizungumza tatizo au kero inayowasumbua kiasi cha kufanya msielewane.

*Kama kuna umuhimu, wa kupinga hoja ya mwenzako, basi fanya hivyo kwa upendo. *Ndugu yangu mmeoana kwa maana kwamba mnapendana, ni vizuri mshirikishe mwenzake mipangilio yako ya kila siku.

Zaidi ya yote jitahidi kutokasirika au kuendekeza tabia za kununa-nuna, kuna tatizo lizungumzwe yaishe.

Ambacho nataka kifahamike katika makala haya ni kwamba matatizo ni sehemu ya maisha, ndoa kama ndoa ni sehemu ya maisha, elewa kuwa utakuwa na mikwaruzo ya hapa na pale, cha msingi ni kujua namna ya kusuruhisha kasoro hizo, hatimaye muweze kwenda sawa.

Siri moja ya msingi sana katika maisha yetu ni kuhakikisha tunakuwa na mawazo kwamba inawezekana. Ukiamini, kwanza ni jambo la msingi, halafu mambo mengine yanafuatia. Ukiamini kwa uhakika kwamba nataka kuwa fulani, kisha ukaanza kuchukua hatua za kuelekea kule ambako unataka, kwa hakika hakuna jambo ambalo litakushinda.

Ninachotaka kieleweke hapa ni kwamba msingi wa maisha ya watu wengi ni nafsi zao, kama unakata tamaa, ndio kusema ni sawa na kifo, ni sawa na kusema aaah basi inatosha, kwa hiyo inakuwa ni mwisho wa kuendelea kuwaza tofauti juu ya kile ambacho umekuwa ukikiwaza.

Wakati fulani miaka minne iliyopita niliwahi kukutana na jamaa mmoja akawa anaomba ushauri juu ya namna gani anaweza kufanya ili kuhakikisha anaishi vizuri kwenye ndoa yake hasa baada ya kumfuma mkewe akiwa na wanaume wengine katika nyakati tofauti wakifanya ngono.

Watu wengi wanapokuwa kwenye uhusiano na wanapoona wenza wao labda wamekuwa na uhusiano na mtu au watu wengine, wanafikiria kutalakiana, lakini huko ni kukosea, unapaswa kukaa naye na kuzungumza naye, ili kujua msingi wa yeye kuwa vile, kisha angalieni mbele, namna gani mnaweza kwenda mbele katika hali ya mafanikio.

Kabla ya kuwa naye, kwa watu walio wengi ni kwamba waliwahi kuwa na watu au mtu mwingine, ni kweli inauma kusikia au kuona ana mwingine, lakini si sahihi kufikiria kutalikiana, cha msingi ni kukaa na kuangalia ni namna gani uhusiano wenu unaweza kuendelea kuwa mzuri, kwa kuondoa msingi wa mmoja kuwa hivyo, yaani kuanzisha uhusiano na mtu mwingine.

Katika uhusiano kuna mambo mengi ambayo unapaswa kuyazingatia, lakini leo tutayaangalia mambo 20, ambayo naamini kwamba kama kweli utayafanyia kazi kwa dhati, kwa hakika uhusiano wako utakuwa mzuri na wenye kuvutia, wala hutakuwa na majonzi tena, baadhi ya mambo hayo ni yafuatayo;

1. Ufanye ubongo wako kutafakari kwa makini yale malengo ambayo umekuwa ukiyawaza kabla ya kuoana kwenu. Je, umewahi kutaka ndoa ya namna gani na sasa unafanya nini?

Waza namna gani unaweza kuwa na ndoa nzuri. Kwa hakika ukifikiria hilo, utafanikiwa. Maisha yetu yanajengwa na fikra, ukiwaza mabaya, utapata mabaya, ukiwaza mazuri, kwa hakika utayapata.

2. Kama kwa mfano ndoa yako tayari imeingia shida, endelea kutafakari kwanini ina matatizo na nini nifanye iwe nzuri?

3. Zaidi, penda kufanya mazuri kwa mwingine, acha kuwaza aaah mbona mimi namfanyia mazuri, halafu yeye ananifanyia mabaya. Endelea kufanya mazuri mengi kwa mwenzi wako hata yeye anaonekana kufanya mabaya, hatimaye naye atakuwa mzuri, kwa maana ya kukufanyia mazuri pia.

Atawaza aaah huyu mtu mbona namfanyia mabaya tu, wakati yeye ananifanyia mazuri, mwishowe atabadilika, ndivyo inavyoaminika kitaalam.

4. Mfanye mwenzi wako ajione ni mwenye thamani na umuhimu mkubwa katika maisha yako. Je, unamthamini mwenzi wako? Tafakari, chukua hatua.

5. Mara zote tafakari ni nini ambacho nikimueleza mwenzi wangu atakuwa mwenye furaha?

6. Tafakari kabla ya kufanya au kuzungumza jambo. Wengi wa watu wanaharibu uhusiano kwa midomo na mikono yao, wakati mwingine unaweza kufikiri unamfanyia mtu kitu kizuri, kumbe sio.

Ni vizuri sana kulizingatia hili. Wakati mwingine kama huna la kuzungumza, ni vizuri kukaa kimya, kuliko kuzungumza 'utumbo'.

7. Shukuru kwa kile unachofanyiwa. Wakati mwingine yawezekana mwenzi wako anakufanyia kitu au anakununulia kitu, hata kama hukipendi, mshukuru kisha sema;
Lakini ukininunulia na kitu Fulani siku ukipata fedha nitapenda pia Usionyeshe kudharau, hata kama labda amekununulia kitu ambacho kutoka moyoni hujapenda.

8. Uwe msikilizaji mzuri. Tena wakati mwingine kama mwenzi wako anazungumza jambo, tulia msikilize hata kama labda ulikuwa unachezea simu nk. Ni makosa makubwa kwa mfano mwenzi wako anazungumza halafu wewe uko bize na kitu kingine ambacho labda wakati huo si cha lazima kukifanya.

9. Jali hisia za mwenzi wako.

10. Acha kauli za kulaumu au kutusi waziwazi, kama mwenzi wako amekukosea, pata muda wa kukaa naye faragha. Ni makosa makubwa kumtusi au kumsema mtu waziwazi, hapo ndipo huzaliwa mabaya mengi, baadhi yake ni vile unaweza kuona watu wakati fulani wakipigana waziwazi
kitaalam watu huwa hawako tayari kudharauliwa hadharani.

11. Acha kuwaza mambo yasiyowezekana. Kwa mfano ni makosa kuamini kuwa katika ulimwengu huu unaweza kumpata mwanamke au mwanaume ambaye ni msafi au mzuri asiye na makosa kwa asilimia mia. Kama unafikiria hilo, ni vizuri ukakaa pasipo kuoa au kuolewa, kwa sababu hayuko, hata Mungu anajua hilo.

Wakati mwingine baadhi ya mambo si makosa, bali yako tofauti na vile ambavyo tungependa iwe, kwa mfano wako watu wangependa kuona dunia haijaumbwa kama hivi ilivyo leo nk, japo ndio uamuzi wa Mungu.

12. Usitoe menno yenye kusababisha maumivu. Kama inatokea mwenzi wako anazungumza maneno yenye kusababisha maumivu, zungumza maneno mbadala, usikuze maumivu. Ongeeni kama watu mliokomaa, acheni kuendekeza migogoro.

13. Zifahamu vema tabia za mwenzi wako na namna gani unaweza kufanya ili kuhakikisha uhusiano wenu unakwenda mbele.

14. Badala ya kuwa na kitabu cha makosa ambayo mwenzi wako anayafanya, ni vizuri ukawa na daftari la mambo mazuri, ambayo mwenzi wako anakufanyia. Tafakari mazuri, zaidi kuliko makosa.

15. Andika tabia nzuri za mkeo au mumeo, badala ya labda sura yake mbaya nk.
16. Angalia ni namna gani unaweza kumfanya mwenzi wako kuwa na tabia nzuri zaidi ya alivyo sasa.

17. Uwe tiba kwa matatizo ya ndoa na uhusiano wenu kwa ujumla. Acha tabia ya kulalamika, kuipiga kelele ovyo.

18. Kumbukeni nyakati zile za furaha na fikra ambazo mmekuwa nazo kuhusu uhusiano wenu. Ongezeni manjonjo yale ya kupendana, na si kufikiria mabaya tu kama ilivyo kwa baadhi ya watu.

19. Angalieni ni namna gani mnaweza kushirikiana katika kuimarisha uhusiano wenu, pia angalieni namna ya kushirikiana katika kazi mbalimbali hasa biashara nk.

20. Ishi kana kwamba unakufa kesho. Mabaya yaliyofanyika jana acha yabaki kuwa ya jana, wala msiyape nafasi kuendelea kuwaumiza vichwa na akili zenu.

Waza leo na kuendelea mbele, achana na jana. Kumbuka watu walikuwa wanatambaa, leo ni watu wazima wanatembea, maisha ni mabadiliko, mtu anaweza kuwa mbaya leo, kesho akawa mzuri, na kinyume chake


NINATEGEMEA KUWA KWA YEYOTE MWENYE MAWAZO ZAIDI KUHUSU HII KITU AYATOE ILI KUWAPA MWANGA WENGINE AU WENZETU AMBAO WANATEGEMEA KUVUTA JIKO!!!! AU VIPI? KAZI KWENU.

No comments: