Wednesday, July 15, 2009

mkuu wa majeshi wa sauzi ziarani bongo
JK akimkaribisha Ikulu Mkuu wa Majeshi ya Afrika ya kusini Jenerali Godfrey Ngwenya wakati yeye na ujumbe wake walipomtembelea ikulu jijini Dar leo
JK akipokea zawadi kutoka kwa mkuu wa Majeshi ya Afrika ya Kusini jenerali Godfrey Ngwenya wakati alipomtembelea ikulu jijini Dar leo.Klia ni mkuu wa Majeshi ya Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange.

JK akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa majeshi ya Afrika ya kusini Jenerali Godfrey Ngwenya(kushoto), Mkuu wa Majeshi ya Tanzania Jenerali Davis Mwamunyange(kulia) pamoja na maafisa waandamizi wa majeshi ya Afrika ya kusini na Tanzania ikulu jijini Dar


JENERALI NGWENYA AISHUKURU TZ
Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini (SANDF), Jenerali Godfrey Ngwenya ameishukuru Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika ukombozi wa Bara la Afrika.

“Tanzania ilitoa mchango mkubwa siyo tu katika ukombozi wa Afrika Kusini, bali katika kulikomboa Bara la Afrika,” Jenerali Ngwenya amemwambia Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Jenerali Ngwenya ametoa shukurani hizo kwa Tanzania wakati yeye na ujumbe wake ulipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete, leo, Jumanne, Julai 14, 2009, Ikulu, Dar es Salaam.

Jenerali Ngwenya amemwambia Rais Kikwete jinsi Afrika Kusini inavyothamini mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Afrika Kusini na nchi nyingine hasa zile za Kusini mwa Afrika.

“Tunapokuja Tanzania, kwa kweli tunarudi nyumbani. Tumeishi hapa, mlituhifadhi sote hapa iwe ni ANC, PAC, Frelimo, ZAPU, ZANU…kila mtu alikuwa hapa,” amesema Jenerali Ngwenya na kuongeza:

“Tunashukuru na kutathmini mchango wa Tanzania katika kutuwezesha kufikia malengo yetu,” amesema Jenerali Ngwenya katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange.

Naye Rais Kikwete amemweleza Jenerali Ngwenya kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhifadhi historia ya ukombozi na vyama vya ukombozi kama ilivyotokea katika Tanzania.

“Shughuli zote za vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika zilianzia pale Kongwa, kabla ya kusambaa katika maeneo mengine ya nchi yetu…hii ni historia ya heshima sana katika nchi na bara letu…hivyo tutahakikisha kuwa tunaihifadhi historia hiyo,” amesema Rais Kikwete.

Ameongeza kuwa kama inawezekana vyama vilivyopigania uhuru kutokea Tanzania na Serikali ya Tanzania vinaweza kwa pamoja kuanzisha aina ya taasisi ya elimu ambayo itaendeleza historia hiyo yenye heshima kubwa.

Jenerali Ngwenya na ujumbe wake aliwasili nchini jana, Jumatatu, Julai 13, 2009, kwa mwaliko wa Jenerali Mwamunyange kwa ziara ambako atatembelea maeneo mbalimbali yanayohusiana na historia ya ukombozi na yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini katika nyanja ya ulinzi na usalama.

No comments: