Friday, July 17, 2009

Askofu Kilaini: Kingunge anajadili hewa kuhusu mwongozo
*Asema kanisa litazidi kuusambaza nchi nzima

Na Leon Bahati

KANISA Katoliki Jimbo la Dar es Salaam limesema kauli ya mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru ya kulitaka kanisa kufuta mwongozo wake kwa wananchi juu ya namna ya kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu ujao, ni ya hewani kwa kuwa haijajadili hoja yoyote iliyo kwenye waraka huo.

Isitoshe, limesisitiza kuwa Kanisa Katoliki halitaufuta mwongozo huo na badala yake litaendelea kuuchapisha na kuusambaza kote nchini, ili elimu hiyo ienee kwa watu wengi.

Askofu msaidizi wa Jimbo la Dar es salaam, Methodius Kilaini alisema jana katika mahojiano na gazeti hili kwamba, anamheshimu sana Kingunge Ngombale Mwiru kwa sababu ana mengi mazuri ambayo amelifanyia taifa hili.

Lakini akasema kuwa katika kauli aliyoitoa bungeni juzi kwamba Kanisa Katoliki lifute mwongozo wake, haina nguvu kwa sababu haikosoi kipengele chochote cha taarifa hiyo bali inatoa maelezo ya jumla.

Alisema kanisa lingeweza kumsikiliza na kuipima kauli yake kama angekuwa amechambua vipengele anavyoona havifai na askofu huyo akaongeza kuwa anaamini kuwa haiwezekani kwa Kingunge kuukosoa mwongozo wote.

“Tunatakiwa tufike mahali tujibu jambo hili kwa hoja. Labda wangesema pale waliposoma kwenye mwongozo huu ingepasa kuwa hivi, na akatoa hoja ili tuendane na hoja," alisema Kilaini.

"Kwa jinsi hiyo tungepata hoja ya Wakatoliki, tungepata hoja ya vyama vya siasa... kuna NGO nazo zingetoa hoja, kuna vikundi na madhehebu ya dini nayo yangetoa pia maelezo yao.

“Tusichanganye (mwongozo) wote kwa pamoja bali zitolewe hoja. Pale penye hoja nzuri ndio patashinda. Twende kwa hoja na siyo kusema tuutoe (mwongozo). Hii hapana.”

Alishangazwa na kitendo cha Kingunge na hata wanasiasa wengine kuujia juu mwongozo huo wakati kanisa limekuwa na utamaduni wa kutoa taarifa za namna hiyo tangu mwaka 1912, na hakukuwepo mtu aliyejitokeza kupinga.

Alifafanua kuwa taarifa hiyo si waraka wa kichungaji kama inavyoelezwa na watu wengi bali ni mwongozo uliotolewa na Wataalamu wa Taasisi ya Kanisa Katoliki (CPT) na kuridhiwa na kanisa.

Alifafanua kuwa waraka huo hawaulengi waumini wa Kanisa Katoliki peke yake, bali wananchi wote bila kubagua dini.

Pia alisema kuwa mwongozo huo haujakiuka taratibu za nchi kama baadhi ya wanasiasa wanavyouelezea kwamba unachanganya dini na siasa na wala hauwezi kuligawa taifa bali unahimiza mshikamano.

“Umeandikwa kwa ajili ya watu wote wenye mapenzi mema. Na wala hakuna kipengele hata kimoja kinachosema waumini wa Kanisa Katoliki wafanye hivi na hivi,” alisema akielezea kuwa unawaelimisha wananchi juu ya sifa za mtu ambaye ni kiongozi bora.

Aliongeza kuwa Kanisa Katoliki halifungamani na chama chochote cha kisiasa na lina imani kuwa mtu yeyote bila kujali dini wala kabila anaweza kuliongoza taifa ili mradi awe ni mwadilifu.

Askofu Kilaini alifafanua kuwa maaskofu, mapadri na watawa wa kanisa hilo si wanachama wa chama chochote cha siasa.

Tofauti na miaka mingine, Kilaini alisema kuwa mwongozo wa wakati huu umeonekana kuwachanganya wanasiasa wengi kwa sababu umegusia suala la ufisadi.

Kilaini alisema kuwa waraka huo hauwezi kufutwa labda kama kuna kipengele ambacho kitaonekana kuwa kina kasoro na kanisa kukiridhia, ndicho kinaweza kubadilika.

Alifafanua kuwa mwongozo huo ambao upo kwenye kitabu chenye kurasa 95, umekuwa ukinunuliwa kwa wingi sehemu mbalimbali nchini.

Kutokana na hali hiyo, Kilaini alisema wanaendelea kuchapisha kwa wingi na kuusambaza kote nchini ili kutekeleza kiu ya watu wengi ambao wanauhitaji.

Aliweka wazi kuwa kasi ya manunuzi imeongezeka baada ya baadhi ya wanasiasa kuushutumu.

Exuper Kachenje na Anna Lusana wanaripoti kuwa jopo la masheikh na wanazuoni, wamekemea vikali kile walichokiita tabia ya baadhi ya madhehebu ya dini kuchanganya dini na siasa.

Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari waliotaka kujua iwapo watatoa waraka kuelekeza kiongozi anayefaa kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu kama lilivyofanya Kanisa Katoliki, katibu wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Khamis Mattaka alisema jopo hilo linakemea vikali tabia ya baadhi ya madhehebu hayo na viongozi wake kuchanganya dini na siasa.

Alisema kimsingi jopo hilo linaelekeza kiongozi kuchaguliwa kutokana na Utanzania wake na siyo kigezo cha dini yake.

"Sisi tulishakemea tabia ya kuchanganya dini na siasa katika kikao chetu cha kwanza mwezi uliopita, leo tunakemea tena kuchanganya dini na siasa," alisema Mattaka na kuongeza;

"Tunataka watu wachaguliwe kwa Utanzania wao na sifa walizo nazo na si kigezo cha dini."

Aliongeza kuwa iwapo mtu yeyote anataka kugombea uongozi, basi auze sera za chama chake kwa wananchi badala ya kutumia mwavuli wa dini.

Wakati huo huo Daniel Mjema anaripoti kuwa mkongwe nchini, Peter Kisumo amemjibu mwanasiasa mwingine mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru kuhusu waraka wa Kanisa Katoliki, akisisitiza kanisa hilo halipaswi kukemewa kama vile limefanya makosa.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kisumo alipinga kauli ya Kingunge kuwa waraka huo unaweza kuigawa nchi kama Lebanon, akisema hilo haliwezi kutokea kwani Lebanon ina vyama vya kidini wakati Tanzania ina vyama vya siasa.

Kisumo aliyewahi kushika nyadhifa kadhaa za juu katika serikali ya awamu ya tatu, alisema kilichopaswa kufanyika ni kwa vyama vya kiraia kuchukua jukumu la kutoa elimu ya kiraia badala ya kuliachia kanisa moja moja kufanya hivyo.

“Ninaamini Kanisa Katoliki limesukumwa kutoa mwongozo huo wakati huu tukielekea katika uchaguzi kwa sababu vyama vya kiraia vimekaa kimya… lakini tusiliachie kanisa peke yake kufanya kazi hii,” alisisitiza Kisumo.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo alikiri kuwa kama vyama vya siasa na serikali vitaachia makanisa pekee kutoa elimu hiyo ipo hatari kubwa ya kusababisha mfarakano, lakini si kwa kiwango kama cha nchi ya Lebanon.

“Kazi hii ya kutoa elimu ikiachwa ifanywe na kanisa pekee inaweza kusababisha mfarakano, lakini hatuwezi kulikemea Kanisa Katoliki kuwa limefanya makosa kwa sababu serikali na vyama vyetu vimekaa kimya, nani aelimishe umma,” alihoji.

Kisumo alisema mazingira ya Tanzania ya sasa yanadhihirisha kuwepo kwa mbegu mbaya iliyoanza kupandwa na ambayo inaweza kuvuruga umoja wa kitaifa kama hoja za kisiasa zitaachwa zishughulikiwe na vyombo vya dini.

“Iko mbegu imeshaanza kupandwa ambayo inaweza kuvuruga umoja wetu na mbegu hiyo itaweza kustawi tu kama hoja za kisiasa hazitashughulikiwa na vyombo vya kisiasa na ikaachwa ishughulikiwe na vyombo vya dini,” alisema.

Kisumo alisema idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza katika chaguzi ndogo za Tarime, Mbeya na Biharamulo ni kielelezo tosha cha kuonyesha mwamko wa wananchi umeshuka na akashangaa vyama vya siasa kutoliona hilo.

Alivitaka vyama vya siasa vikiwamo CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kuichukua agenda ya kutoa elimu ya uraia kama hiyo kwani ndivyo vyombo vya kiraia.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni juzi, Kingunge aliushambulia waraka huo unaoelezea namna ya kupata kiongozi anayefaa katika uchaguzi ujao.

No comments: