Monday, October 25, 2010

mgambo wa jiji kutumia kulinda vituo vya kupigia kura siku ya uchaguzi mkuu

Na Mohammed Mhiona, wa Jeshi la Polisi

Wakurugenzi wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam wamesema watawatumia Askari Mgambo katika kusaidiana na Jeshi la Polisi katika kulinda Usalama wa vituo wakati wa zoezi la upigaji kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Wakurugenzi hao waliyasema hayo wakati wa mkutano wa pamoja na Makamanda wa Polisi wa Mikoa mitatu ya Kanda ya Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo wametoa wito kwa kila askari mgambo kupiga ripoti kwa mshauri mgambo wa wilaya yake.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ilala Bw. Gbriel Fuime, na Mkurugenzi wa wilaya ya Temeke Bw. Stephen Kongwa, wamesema kuwa mgambo hao watakuwa sehemu ya walinzi wa vituo na watalipwa posho kama ilivyotagazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Wamesema Mgambo hao watahakikiwa na kupangiwa kazi na baadaye kutawanywa katika vituo watakavyopangiwa na wakurugenzi katika halmashauri husika.

Awali Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Naibu Kamishna (DCP) Suleimani Kova, Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Absalom Mwakyoma, na Msaidizi wake ACP Charles Kenyela, walisema ni vema kila kukijitokeza jambo la muhimu, kuvitumia vyombo vya habari katika kutoa ufafanuzi ili kuwaondolea wananchi shaka katika mambo ya kuhiisi.

Mkutano huo pia umewashirikisha maafisa waandaamizi kutoka mikoa hiyo pamoja na wakuu wa Upelelezi wa mikoa hiyo.

No comments: