Wednesday, February 18, 2009





MWANAMUZIKI mahiri wa Msondo Ngoma, Joseph Maina amefariki ghafla jana asubuhi akiwa ndani ya daladala.
Dereva wa basi la daladala lenye namba za usajili T582 AFL linalofanyika safari kati ya Mwenge na Temeke Mikoroshoni, Kassim Salum aliiambia Mwananchi jana kwenye Hospitali ya Temeke kuwa msanii huyo alifariki akiwa amekaa kiti cha mbele mlangoni.
"Unajua aliwahi kuingia, na sisi ilikuwa zamu yetu kupakia hapo Temeke Mikoroshoni, kulikuwa na abiria anataka kupanda, nilipomwambia asogee kiti cha kati, nikaona anakakamaa na muda mfupi akalala.
"Baada ya kuona hali ile, watu walijaa na niligeuza gari hadi kituo cha polisi Maghorofani, lakini na wao walinipa askari wakaniambia tuelekee hospitali ya Temeke," alisema Salum.
Hata hivyo, mwili wa Maina ulibakia kwenye kiti cha daladala kwa takriban saa nzima katika hospitali hiyo huku mashabiki na watu wengine wakielezea kumfahamu kama ni Maina. Mwananchi ilifika hospitalini hapo na kukuta umati wa watu wakielezea masikitiko yao kutokana na kifo hicho.
Saa 7:11 mchana, kiongozi wa Msondo Ngoma, Muhidin Maalim Gurumo aliiwasili akifuatana na mpiga solo, Said Mabera, wacheza shoo na wanamuziki wengine.
Hata hivyo, wasimamizi wa chumba cha maiti walimruhusu Mabera kwenda kutambua mwili na aliporudi alithibitisha kuwa kweli ni Maina.
Gurumo alisema kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na miguu na bendi walikuwa wakiandaa utaratibu wa kumtafutia matibabu.
"Kwa kweli ni pigo kubwa kwani Maina alishiriki katika nyimbo zote za Msondo, alishiriki albamu zote ni pigo kwa sasa hatuna la kusema tutatoa taarifa," alisema.
Maina ambaye ameacha mke na watoto wa wawili alitunga kibao kumuimbia mke wake, Mama Cossy ambacho hakijatoka.
Maina ameongeza pengo la wanamuziki wakali wa bendi hiyo waliofariki miaka ya karibuni, akiwemo TX Moshi William, Athumani Momba na Suleiman Mbwembwe.

No comments: