FIFA World Cup trophy jets into Tanzania
The First Family pose with the trophy
President Jakaya Kikwete holds the FIFA World Cup Trophy at the NAtional Stadium in Dar es salaam today. Right is FIFA representative Hadi Amal and left is Coca Cola Tanzania Marketing Manager Herrieth Mutayobwa. Hundreds of soccer fans turned up at the stadium to witness the coveted troph and some had the chance to have their photos taken while standing near it.
First Lady Salma Kikwete is happy to hold the trophy
Your Excellency... Sorry. Its you, only you, who is allowed to touch the trophy...
President Jakaya Kikwete holds aloft the trophy
dancers entertain
a police chopper was but one of the many security measures taken to guard the trophy
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE KWENYE UZINDUZI WA ZIARA YA KOMBE LA FIFA LA DUNIA UWANJA WA TAIFA DAR ES SALAAM 19 NOVEMBA, 2009
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Joel Bendera (Mb;
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Chiku Garawa;
Waheshimiwa Wabunge;
Wawakilishi wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA;
Viongozi wa Kampuni ya Coca-Cola;
Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF;
Wageni Waalikwa;Mabibi na Mabwana
Najisikia mwenye furaha kubwa kupata fursa hii ya kujumuika nanyi katika tukio hili la kihistoria kuhusu ziara ya Kombe la FIFA la Dunia hapa Tanzania.Nchi yetu imebahatika, kwa mara nyingine tena, kupata ugeni huu mkubwa wa Kombe la FIFA la Dunia ambayo ndiyo tuzo ya juu inayotolewa kwa nchi bora kuliko zote katika soka duniani. Hii ni mara ya pili sasa kwa FIFA kutupa heshima hii. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2006.
Napenda kuwashukuru FIFA na Coca- Cola kwa upendeleo huo kwa nchi yetu.Kabla ya FIFA na Coca-Cola kuanzisha ziara ya Kombe la FIFA la Dunia, wapenda soka wengi duniani walikuwa wanaliona kombe hili kupitia kwenye picha za magazeti na luninga.
Leo hii kupata bahati ya kuliona kombe lenyewe “live” ni jambo la kihistoria litakalodumu katika kumbukumbu yetu kwa miaka mingi. Naipongeza FIFA kwa kuanzisha utaratibu huu wa kuwezesha maelfu ya wapenda soka duniani kuliona kombe hilo kwa karibu na wengine hata kupata nafasi ya kulishika na kupiga nalo picha.
Hii ni fursa ya pekee na ya kujivunia. Kwa Watanzania wenzangu tuichukulie ziara ya Kombe la Dunia nchini mwetu kama ni changamoto kubwa kwetu inayotutaka tufanye vizuri zaidi katika soka ili tulingane nayo heshima hii tuliyopewa.
Hasa ni changamoto kwa viongozi wa soka wa ngazi zote pamoja na wachezaji na wapenzi wa mpira wa miguu nchini. Kuja kwa kombe hili ni deni kwetu na kulilipa kwetu sisi ni kuzinduka, tuendeleze kiwango chetu cha soka nchini ili na sie siku moja tushiriki fainali za kombe hili.
Hili ni jambo linalowezekana. Wapo wenzetu Afrika wameweza, kwa nini sisi tusiweze. Wao ni watu kama sisi, maadamu wameweza na sisi tutaweza. Lakini, ili tuweze hatuna budi kuiga mfano wao hususan waliyofanya na wanayoendelea kufanya kuendeleza mpira wa miguu. Twende tukajifunze kutoka kwao.
Lakini hata kabla ya kwenda huko, yapo mambo ambayo hatuna budi kuyafanya. Naomba nitaje baadhi yake:-
1. Tuimarishe uongozi, utendaji na uendeshaji wa vilabu vya mpira. Mchezaji hufundishwa kucheza mpira katika klabu yake. Hapo ndipo hufundishwa maarifa ya kucheza mpira na vipaji kuendelezwa. Hebu tujiulize hali ya vilabu vyetu vya soka nchini ikoje.
Je vinaongozwa vizuri? Vinaendeshwa vizuri? Jibu tunalijua sote kwamba ni hapana. Lazima suala hili tulitafakari kwa yakini na kulipatia jawabu. Tukishindwa kupata jawabu muafaka na mambo yakaachwa kuendelea yalivyo, mpaka mwisho wa dunia hatutakuwa tumesogea popote.
2. Tupate walimu wenye ujuzi na uzoefu kufundisha timu zetu. Hii ndiyo njia ya uhakika ya kukuza na kuendeleza vipaji na hivyo kupata wachezaji walio bora.
3. Tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka umri mdogo. Vilabu viwe na timu za watoto na vijana. TFF isaidie kuanzishwa kwa shule za mchezo wa mpira wa miguu kwa watoto na vijana. Mashuleni wapatikane walimu wa michezo walio wazuri kufundisha.
4. TFF ionekane zaidi ya ilivyo sasa katika mipango ya kuendeleza soka mashuleni, vijijini, mitaani na hata vilabuni. TFF ikiwa na mipango na ikasimamia na kuwabana wadau kuitekeleza itasaidia. Vinginevyo TFF itabakia kusimama ligi kuu, kutoa adhabu kwa wachezaji, na timu ya taifa.
Hiyo haitoshi.Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi kwa kampuni ya Coca-Cola kwa mchango wake muhimu inaotoa kuendelea mchezo wa soka nchini na hasa soka la vijana. Mashindano ya Kombe la Copa Coca-Cola kwa vijana wa chini ya miaka 17 ni ushahidi tosha wa mchango huo adhimu.
Mashindano hayo yamegusa vijana wengi kote nchini. Naambiwa zaidi ya timu 1500 zilijitokeza kwa mwaka huu na maelfu ya vijana walijitokeza kuonyesha vipaji vyao. Naomba utaratibu huu uendelee kwani utakuwa na manufaa makubwa siku za usoni.
Maombi yangu kwa TFF ni kujipanga vizuri kutambua vijana wenye vipaji vizuri na kupanga mipango ya kuiendeleza.Ujio kwa Kombe la FIFA la Dunia hapa nchini mbali na kuhamasisha vijana wetu pia ni fursa nzuri ya kutangaza nchi yetu pamoja na fursa zake za utalii na uwekezaji.
Watu wengi zaidi wataifahamu nchi yetu vizuri zaidi kupitia ziara hii ya Kombe la Dunia. Hivi sasa tuna uwanja mpya wa kisasa ambao utaonekena vizuri wakati wa ziara hii na pengine kuvutia timu kubwa duniani kuja kufanya mazoezi hapa wakati wa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Afrika Kusini 2010.
Changamkieni fursa hii kwa maslahi ya taifa letu ili tunufaike na sisi. Baada ya kusema maneno haya machache, sasa niko tayari kufanya kazi iliyotuleta hapa sote. Nawashukuruni kwa kunisikiliza.