Saturday, June 4, 2011

Mnasubiria bajeti ya kuwaletea maisha bora?

Mzee wa Kujitoa

NASIKIA wiki ijayo ndipo mtakapotusomea bajeti. Mzee wa Kujitoa natamani ningekuwa ndiye ninaandaa hiyo bajeti. Bajeti inayoandaliwa na serikali iliyokuwepo madarakani tangu uhuru unatarajia yatakuwepo yapi mapya? Kwani baada ya kuambiwa kwamba mnaletewa maisha bora kwa kila mmoja wenu ipo siku mlishaona bajeti ya kuwaletea hayo maisha bora? Miye simo ila nawaapia msiwe na ndoto ya maisha bora kwa bajeti inayotarajia kuwasilishwa.

Mtakuwaje na maisha bora wakati hawatakuwa tayari kupunguza fedha kwenye fuko la matumizi ambayo sisi twadhani siyo ya lazima? Maisha bora yatakuja vipi wakati wanagoma posho za wabunge zisiondolewe? Kuna mijitu inashangaza kinoma, eti wanasema posho ni lazima kwa kuwa wabunge wanafanya kazi.

Nani kakataa kwamba wanafanya kazi? Lakini si wanalipwa mishahara kwa kufanya kazi? Na kazi yao si pamoja na kuhudhuria vikao vya bunge? Wapo wachache wanaolalamika kwamba kuna gharama za malazi. Ikifika hapo nadhani tuwajengee hosteli tu walale huko wabunge wote huko.

Posho ya kikao wakati kikao ni sehemu ya kazi? Kwani ni siri kwamba kuna maofisa wengi wa serikali wanamaliza muda mrefu kwenye vikao vyenye posho wakati wameajiriwa pamoja na mambo mengine kufanya hivyo vikao. Mnashangaa sana. Hivi itakuwaje kila daktari akisema kabla ya kudunga sindano au kufanya uapsuaji naye anataka posho?

Wakili kabla ya kukanyaga kortini naye aseme anataka posho? Mwalimu kabla ya kuingia darasani naye atake posho? Si mmeamua kwamba kila kazi inahitaji posho inayojitegemea mbali na mshahara? Kwa mtaji huo mnatarajie muwe na bajeti itakayowanyanyua walalahoi? Mie huko simo kabisa watu wangu. Simo!

Mnatarajia bajeti itakayowaletea maisha bora kwa mbwembwe hizi za wakubwa? Eti unahitaji mtoyota mkubwa kama Vx kukutoa Mbezi au Masaki kwenda ofisni mtaa wa Samora? Si huo kama si upotevu wa fedha mwadhani ni kitu gani? Kwani hamjui kwamba migari hii inanyonya mafuta kama haina akili nzuri vile?

Wanaochimba mafuta wenyewe wala ahawaitumii kwa kiwango chenu. Bila kuwa na bajeti itakayoweka kando matumizi yasiyo yala zima ya magari ya kifahari na kuzuia ununuzi wa magari mapya ujue imekula kwetu. Wacha nijitoe humo.

Kama hamna nyongeza ya mshahara inayoendana na hali ya maisha bajeti ijayo itaacha kuwa ya majonzi kwenu? Nawauliza enyi walimwengu, bei ya unga wa mahindi ni shilingi ngapi leo? Kwa wengi wetu siku hizi nyama ishakuwa ni anasa, labda tuzikute kwenye sherehe au kwenye sambusa ya nyama. Nani anamudu leo kununua kilo ya nyama kwa huu mshahara wa sasa?

Kijiweni kwetu tayari wanaita nyama ni chakula cha kifisadi. Hapo sijazungumzia sukari na mafuta ya kupikia. Nazungumzia haya ya kupikia tu, hayo ya petrol na dizeli nikiyafikiria natetemeka. Huko simo miye.

Nasema kaeni mmejikunyata mkisikiliza bajeti lakini siwapi moyo wa matumaini. Unadhani katika bajeti hii kutakuwa na nyongeza katika matumizi ya dispensary ya kijijini kwenu? Kwani mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi? Miye simo. Jiandaeni kufika kwenye vituo vya afya na haspitali na kukuta bohari za dawa zikiwa tupu. Mbona tushazoea hali hiyo? Sana sana kitakachoongezeka kipya ni fedha za kununulia bajaji za akina mama wajawazito. Hiyo naona ndio ahadi rahisi zaidi kutekelezeka.

Kama kwa mawazo yenu mnatarajia kuona bajeti ya mwaka huu ikionyesha utekelezaji wa ahadi za kampeni naamini mnajisumbua. Kwamba katika bajeti hii tukute huko fedha za kununua meli mpya, kujenga viwanja vya ndege na mambo kama hayo? Nasema sahau, isitoshe bado kuna miaka mingine minne! Mnabisha hata hilo? Sisi si nitaifa changa sasa kinawauma nini kuwa na bajeti finyu?

Kama tungekuwa tumeweza kudhibiti dhahabu yetu na kuitumia wenyewe walau hapo kingeeleweka. Mnazungumzia uwepo wa dhahabu ardhini bila luzungumzia uondoshwaji wa hiyo dhahabu? Mtashangaa sana hadi watu wawashangae kwa nini mnashangaa.
Kumbe ninyi mlitaka eti na ile bajeti ya vitafunwa iondolewe? Hamjui hivyo vitafunwa vinatumika wakati wakubwa wakitafakari namna ya kuwaondolea umaskini katika vikao ambavyo wahudhuriaji wanalipwa posho hata kama ndio kazi yao inayowalipa mshahara? Mnadhani mazingaombwe yamekwisha duniani?
Nawaambia isikilizeni kwa umakini sana bajeti ijayo halafu kando yenu muwe na zile ahadi za uchaguzi uone kama kuna uwiano. Kwani siku zote kuhaidi si ni rahisi kuliko kutekeleza? Mnabisha nini? Kamuulzieni anko Ben alimaanisha nini aliposema sera za chama nambari wahedi hazitekeleziki. Kama kawaida mimi huko simo hata siku moja miye.

Hizi bajeti ambazo zinategemea pia wafadhili nazo zina mizozo yake. Kwani hamjui anayepiga ngoma ndiye anayeamua mdundo? Sasa sisi si tuna miaka 50 ya kuwa huru? Kuwa huru wakati bajeti yetu haiwezi kusimama bila kupitisha kapun kwa wafadhili? Hivi kinachotufanya tuwategemee hao watu wanaojiita wabia wetu wa maendeleo ni kipi hasa? Wana akili kuliko sisi? Wana rasilimali kuliko sisi? Ukitoa jibu sahihi utakuwa katika hatari ya kuwa umetukana. Ngoja nikae kimya kabla hajamipiga makofi.

Bajeti tegemezi inaweza kweli kuwa bajeti ya kuleta maendeleo kwa watu wetu? Mambo mengine ninyi yaoneni tu lakini mistake kuyajua undani wake. Maisha bora yanayotegemea tabasamu la wazungu mbona ni kitu kisiachoaminika kama wingu kwenye upepo? Asiyejua maana usimpe maana, mwenye akili anaelewa. Mimi huko simo kabisa tena wala msiniguse. Sijasema kitu miye.

Siku mkitaka bajeti ya kutubadilisha sisi akina yakhe lazima kwanza ufisadi uwe umetokomea, na maliasili yetu tunaifaidi wenyewe. Naona vuguvugu limeanza, maisha ni makali kinoma lakini panapokaribia kuchwa ndipo usiku unakuwa mzito zaidi. Miye simo kabisa kwenye haya yote wala msinitaje.

1 comment:

MDAUUK said...

Nakubaliana nawe hasa point yako ya watu kuendesha magari yenye CC kubwa. Ni kutafuta ufahari bila ya kutumia akili, kwanini watanzania hatuna hulka ya ku save hela zetu kama labda waingereza?
Gari zenye CC ndogo ni rahisi kupaki mjini, ni rahisi kwa petroli na hazitoi moshi mzito.
Kuhusu swala la posho, siamini mtu uliejiriwa tena kuwatumikia wananchi unaitaji posho ya kuhudhuria mkutano, HUO NI UFISADI! Kama ni hivyo basi hata manesi, madaktari, wasafisha barabara basi na wengineo,basi wadau posho pia? Inaonyesha jinsi ubunge ulivyo deal siku hizi, mtu anaiba au kufanya utapeli kwenye mashirika ya umma nakuzitumia pesa hizo kugombea ubunge! Sijui nchi yetu inaenda wapi!
Bajeti yetu TENA ikajaa posho za mabilioni na hela za vitafunio kwa mabilioni!
Hakuna kusitiza kwa nguvu ununuzi wa magari ya VX wala misafara mikubwa isio nakichwa wala miguu, TENA wananchi tumetapeliwa na kuachwa watupi na viongozi wetu WALAFI!
KAZI TUNAYO!