Laptop ya Nguvu za Jua
Maonyesho
ya wiki ya kimazingira yanayojulikana kama ‘Inhabitants Week in Green’
yanamalizika rasmi leo, lakini hayakupita bila ya kugusa hisia zetu sisi
wapenzi wa gajeti, kampuni ya Fujitsu wameshusha laptop sahihi kabisa
inayoendana na mazingira ya nchi kama Tanzania, hili linatokea tukiwa
bado hatujasahau kwamba si muda mrefu uliopita kule Zanzibar umeme
ulikatika kwa muda wa kiasi cha miezi mitatu.
Kilichotuvutia
sisi wa Gajetek katika laptop hii ambayo haikutolewa habari zake za
kutosha kwa sasa ni mambo mawili. Mosi, laptop hii haihitaji chaja
kabisa kwani inajichaji na paneli zenye kutumia nguvu za jua (Solar
panels) zilizo kwenye eneo linalokaa kibodi na nyuma ya skrini. Pili, ni
kuwa laptop hii bado imeweza kuwa nyembamba na yenye kuvutia mno
kimaumbile huku ikiwa imezungukwa na paneli ya kioo (glass panel).
Hivyo
umeme ukatwe mwaka mzima, wewe unaendelea na kazi zako bila ya kujali
lolote kwa vile laptop hii inajichaji ikiwa inatumika na hata ikiwa
haitumiki. Hivi karibuni Apple wamejigamba kuwa sasa wanaelekea kwenye
hali ya ‘cable free’ wakitumia kauli ya kimatangazo (slogan) ya kata
waya lakini hii ndio laptop ambayo inakupa uhuru wa kuondokana na miwaya
kikweli, kwani gajeti za Apple bado zinahitaji waya ili kuzichaji.
Fujitsu
hawakutoa fununu zozote juu ya ni lini laptop hii itakuwa tayari kwa
mauzo au ina vianisho halisi vya aina gani. Laptop hii inatumia paneli
aina ya photovoltic katika kuichaji na hivyo imeondoa mchukizo wa kisura
na upana paneli za nguvu za jua za kizamani. Pamoja na uchache wa
habari zake laptop hii imevutia wengi, ingawa kwa wenzetu wa nchi
zilizoendelea ni suala la kimazingira tu, kwetu sisi wa nchi
zinazoendelea ni suala linaloendana na hali halisi ya maisha yetu, yaani
kukosa umeme kwa maeneo ya vijijini na kukatika katika kwa umeme kwa
maeneo ya mijini. Tunamalizia kwa kusema hii ni laptop halisia kwa
mazingira ya Tanzania.