Friday, January 6, 2012

Majambazi wavamia ndege ya dhahabu


Pichani: Wakazi wa Wilaya ya Geita mkoani Mwanza, wakiangalia mwili wa mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi (jina hajafahamika), akiwa ni mmoja wa watu wanne waliyovamia mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM), akiwa amekufa baada ya kupigwa risasi na askari polisi katika jaribio hilo la kutka kupora dhahabu jana. (Picha na Sitta Tumma)
WATU wanne wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM), na kuteka ndege ya kubeba madini hayo na kupora vitofali 68 vya dhahabu iliyokuwa ikisafirishwa kutoka mgodi huo kwenda nje ya nchi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 130.

Hata hivyo, majambazi hao walishindwa kuondoka na dhahabu hiyo baada ya polisi wilayani hapa kuwahi kufika eneo la tukio na kuiokoa, baada ya kupambana na majambazi hao kwa
kurushiana risasi na kuua mmoja.

Dhahabu iliyonusurika kuporwa na majambazi hao kwa mujibu wa madai ya mmoja wa polisi aliyeikagua ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, ilikuwa ni zaidi ya kilo 1,000.

Polisi huyo alidai kuwa dhahabu hiyo ilikuwa imegawanywa katika makasha 16 huku kila kasha likiwa na vitofali vinne vya dhahabu na kila kitofali kikiwa na uzito wa kilo 25.

Hata hivyo, Ofisa Madini mkazi wa Kanda ya Geita, Juma Sementa, ambaye ofisi yake imekuwa ikikagua na kuhakiki dhahabu kabla ya kusafirishwa kila wiki na mgodi huo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu uzito kamili wa dhahabu iliyokaguliwa na ofisi yake juzi kabla ya kusafirishwa
jana, alitofautiana na madai ya polisi.

Sementa alisema ofisi yake ilikagua makasha 25 na kila kasha likiwa na kitofali kimoja cha dhahabu chenye uzito wa kati ya kilo tano na 30.

Katika tukio hilo la aina yake, polisi walimuua mtuhumiwa mmoja baada ya kummiminia risasi kifuani, ingawa tayari alikuwa amejeruhiwa na mmoja wa walinzi wa mgodi huo ambaye ni
raia wa Afrika Kusini.

Tukio hilo lilitokea jana saa 5.55 adhuhuri katika uwanja wa ndege wa mgodi huo ulioko umbali wa kilometa tano kutoka katikati ya mji wa Geita.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio na kuthibitishwa na baadhi ya maofisa wa polisi wilayani hapa, uchunguzi wa awali ulionesha kuwa majambazi wapatao
wanne walivamia mgodi huo wakiingilia lango kuu la uwanja huo wa ndege.

Ilielezwa kuwa majambazi hao wakiwa na mabomu ya kutupa kwa mkono, bunduki aina ya SMG na bastola, waliishambulia kwa risasi ndege iliyokuwa ikipakia dhahabu kutoka kwenye gari maalumu.

“Hali hiyo iliwafanya walinzi wa mgodi huo waliokuwa wakilinda usalama wa mali iliyokuwa ikisafirishwa, kutimua mbio, lakini alibaki Mzungu raia wa Afrika Kusini mfanyakazi wa
mgodi huo, aliyekuwa na bastola.

“Raia huyo wa Afrika Kusini alipambana na majambazi hao kwa kuwafyatulia risasi,’’ alisema mmoja wa maofisa wa Polisi katika mahojiano maalumu na gazeti hili.

Ilidaiwa kuwa wakati raia huyo akiendelea kufyatuliana risasi na mmoja wa majambazi hao, aliishiwa risasi na kujeruhiwa kwa kupigwa risasi kwenye mkono na kukimbia kuokoa maisha
yake.

Hata hivyo, baada ya muda mfupi, inadaiwa askari Polisi walifika na kupambana na majambazi hao ambapo watatu walitimua mbio na kubaki mmoja ambaye tayari alikuwa amejeruhiwa
na Mzungu huyo; akashambuliana kwa risasi na polisi, lakini alizidiwa na kuuawa.

Bastola, mabomu, bunduki
Jambazi aliyeuawa bado hajatambuliwa jina na alikutwa na bastola aina ya Chenese namba 0048467 ikiwa na risasi sita, na bunduki aina ya SMG namba UA89381997 inayoonekana kusajiliwa Uganda.

Pia alikutwa na mabomu manne ya kutupa kwa mkono, magazini nne na risasi 60 ambazo hazijatumika, huku akiwa amevalia nguo za kawaida nguo nne ndani na ya juu ikiwa ni sare za
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Jambazi huyo naye alimjeruhi kwa risasi mfanyakazi mwingine wa mgodi huo, raia wa Afrika Kusini aliyetambuliwa kwa jina la Engenas Van Der Schuffs, baada ya kumpiga risasi kwenye mkono wa kulia.

Marubani wa ndege iliyoshambuliwa yenye namba SH-TZX walitambuliwa kwa majina ya Meja Kondo Hamza na Hamdan Salehe.

Hata hivyo, habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio zilisema ndege hiyo ilishindwa kuondoka kwenye uwanja huo kutokana na moja ya mabawa yake kutobolewa kwa risasi.
Chanzo:Habari Leo

No comments: