Watuhumiwa EPA watinga kizimbani  
************
HATIMAYE mafisadi wanaotuhumiwa kuchota mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), jana walifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka ya kughushi na kujipatia mamilioni ya fedha toka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jumla ya watu 10, akiwemo  mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu  Patel, pamoja na wafanyakazi wa BoT walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu.Kesi hiyo ya aina yake ilishuhudiwa na wakazi wengi wa Jiji la Dar es  Salaam na vitongoji vyake ilichukua zaidi ya saa tano na kumalizika saa 11:45  jioni wakati muda wa kazi unaisha saa 10.30 jioni.
 Washitakiwa hao walipandishwa  kizimbani kwa nyakati tofauti huku mshitakiwa namba moja katika kesi hiyo,  Johnson Lukaza akipandishwa peke yake kujibu tuhuma za kula njama na kughushi na  kuiibia BoT zaidi ya Sh6.3 bilioni.Mbele ya Hakimu, Euphemia Mingi, wakili wa  serikali Winie Koroso alidai kuwa, kati ya Desemba 2003 na 2005 mshitakiwa  alighushi hati ya kuhamishia mali toka kampuni ya Kernel na Maruben ya nchini  Japan ambayo ilikuwa inaonyesha imetolewa Februari 4 mwaka 2005.
 Koroso alidai kuwa baada ya  kughushi hati hiyo aliiwasilisha BoT jijini Dar es Salaam na kujipatia kiasi  hicho cha fedha.Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana shtaka hilo na Hakimu Mingi  aliahirisha kesi hiyo mpaka Novemba 18 itakapotoa maamuzi ya dhamana.Katika kesi  nyingine washitakiwa watatu akiwemo Jeetu Patel na ndugu zake wawili Devendra  Patel na Amit Nandy walipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kula njama na  kuiibia BoT zaidi ya Sh 2.5 bilioni.Washitakiwa hao, ambao walifikishwa mbele ya  Hakimu Neema Chusi, kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Agosti 7 na Desemba 7  mwaka 2005 jijini Dar es Salaam walikula njama za kuiibia BoT Sh2,599,944,456.12  na kuziwakilisha katika kampuni ya Matsushita Electric Trading.
 Katika kesi hiyo mshitakiwa wa  tatu Amit Nandi anadaiwa kughushi hati iliyoonyesha kuwa kampuni hiyo ya  Matsushita inaidai BoT kiasi hicho cha fedha.Wakili Koroso aliendelea kudai kuwa  Septemba 2 mwaka 2005 washitakiwa walikula njama ya kuiibia BoT Sh3.9 bilioni  baada ya kusaini mkataba kati ya kampuni ya Bina na C. Itoh za nchini  Japan.Washitakiwa hao walikana mashtaka yao na mahakama imeahirisha kesi hiyo  hadi leo itakapotoa maamuzi ya dhamana.
 Mfanyabiashara huyo mwenye asili  ya Kiasia pia alipandishwa kizambani tena na ndugu zake watatu, wakiwemo wawili  wa awali na Ketan Chohan aliyeongezeka wakikabiliwa na tuhuma za kughushi  mkataba wa Kampuni ya Bina Resort na Itoh wakituhumiwa kula njama na kuibia BoT  zaidi ya Sh3.9 bilioni.Pia wafanyakazi watano wa BoT, akiwemo mtu na mke wake,  walipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kula njama ya kuiibia benki  hiyo.Washitakiwa hao ni pamoja na Bahati Mahenge, Manase Mwakale, Devis Kamungu,  Godfrey Moshi na Iddah Mwakale, ambao kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Desemba  23 mwaka 2003 na Oktoba 26 2005 jijini Dar es Salaam walikula njama za kuiibia  BoT.
 Watuhumiwa hao wanadaiwa kugushi  mkataba wa makubaliano wa kampuni ya Changanyikeni kwa kutumia saini ya meneja  wa kampuni hiyo, Samson Mapunda na kujipatia Sh 8.5 bilioni mali ya BoT, lakini  walikana mashitaka yao na kurudishwa tena rumande hadi leo mahakama itakapotoa  maamuzi ya dhamana.Hata hivyo ni makampuni machache kati ya makapuni  yaliyohusika katika wizi huo ambayo jana yalitajwa kuhusika na wizi  huo.
 Kufikishwa mahakamani kwa  watuhumiwa hao kunatokana na ya mafisadi hao walioshindwa kurejesha sh 64  bilioni kati ya sh 133 bilioni zilizochotwa kwenye akaunti hiyo.Macho ya wengi  yalikuwa kwa mtuhumiwa Jeetu Patel, ambaye alionekana kuwa kigogo pekee kati ya  wafanyabiashara kumi waliofikishwa mahakamani jana.Kilichovutia zaidi ni namna  Jeetu alivyokamatwa. Kukamatwa kwake kunaonekana kulipangwa kisayansi kwa  kutumia mbinu mahiri za kikachero ambazo zilipangwa na Kurugenzi ya Upelelezi ya  Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Jeshi iliyo chini ya Robert Manumba na Ofisi ya  Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP).
 Taarifa ambazo zilipatikana  jijini Dar e s Salaam jana zinasema kukamatwa kwa Jeetu kulifanywa kwa siri  kubwa, kiasi cha mfanyabiashara huyo kutohisi lolote.Duru hizo za kiserikali  zililidokeza gazeti hili kwamba, jana, mnamo saa 4:00, asubuhi Jeetu alipigiwa  simu akaelezwa kwamba anahitajika kwa DPP, Eliazer Feleshi ambaye alikuwa pamoja  na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.Wakati Jeetu  akiwa anasita, alipigiwa tena simu akisisitiziwa kuhitajika kwa DPP na DCI ambao  walikuwa wakimsubiri kwa ajili ya mazungumzo."Alipigiwa simu asubuhi, akaelezwa  kuwa anapaswa kuja kwa DPP na DCI wako wanamsubiri. Mara ya kwanza akawa ana  sitasita kuja; akapigiwa tena kuelezwa kwamba DCI na DPP walikuwa wakimsubiri  hivyo anapaswa kwenda," zilisema duru hizo za kiserikali na kuongeza:"Hakuwa  akijua kabisa kwamba atapandishwa mahakamani. Alivyofika tu akaelezwa anapaswa  kwenda mahakamani kusomewa mashitaka, hivyo ndivyo jinsi alivyokamatwa  Jeetu."Jeetu na makampuni yake tisa anatuhumiwa kujipatia Sh10.3 bilioni kwa  madai ya kutumia nyaraka na kumbukumbu za kughushi, kitu ambacho ni kosa la  jinai.
 Duru nyingine zilisema mbali ya  Jeetu, hata mtuhumiwa Johnson Rwekaza hakuwa akijua bali alipigiwa simu asubuhi  na kuelezwa anapaswa kupanda kizimbani.Duru hizo ziliongeza kwamba, watu wengine  watano wa kampuni ya Changanyikeni Residential Complex, walijisalimisha wenyewe  polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani."Hawa wa Changanyikeni Complex  walijisalimisha wenyewe baada ya kupata taarifa kwamba, wanahitajika kwa ajili  ya kufika mahakamani kusomewa mashitaka," ziliongeza duru hizo.Watuhumiwa hao na  wengine kumi jana walipelekwa rumande na msafara wa magari manne ambao uliondoka  Mahakama ya Kisutu mnamo saa 12:30 jioni huku ukiwa na askari wenye silaha  katika magari mawili aina ya Land Rover, Defender.Msafara huo uliongozwa na  makechero waandamizi ambao walikuwa wametanda katika Mahakama ya Kisutu saa  mbili kabla ya watuhumiwa kufikishwa mnamo saa 7:00 mchana.
 Kufikishwa mahakamani kwa akina  Jeetu ni ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, ambaye alionya kwamba, wafanyabiashara  ambao wangeshindwa kurejesha fedha ifikapo Oktoba 31, walipaswa kufikishwa  kizimbani ifikapo Novemba mosi.
No comments:
Post a Comment