Wednesday, November 26, 2008

Si kila mwanamke unayemwona kanenepa eti ana raha, la hasha!


2008-11-23 12:55:00
Na Anti Flora Wingia

Mpenzi msomaji, bado katika safu yetu hii naendeleza misukosuko wanayopata baadhi ya kinamama wanaotishiwa kupokonywa mali zao na waume zao.

Hebu sikia kilio cha mwenzetu huyu aliyenitumia kupitia barua pepe ya safu hii.

Dada Flora, yupo baba mmoja jirani yangu hivi karibuni ametoa mpya ya mwaka pale alipodiriki kutaka kumchoma kisu mkewe kwa madai kwamba amekataa kumpatia hati ya nyumba.

Nyumba hiyo inavyosemekena imejengwa na mwanamama huyo baada ya kugundua mume hana mwelekeo wowote, licha ya kupata pesa nyingi na kuzimalizia kwenye ulevi na anasa za wanawake.

Mambo hayo yalikuwa ni siri ndani ya muda mrefu moyoni mwa mama huyo ambaye kimuonekano ni mcheshi kwa kila mtu na ilikuwa vigumu kwetu sisi majirani kujua kilichokuwa kinaendelea ndani ya familia hiyo.

Mama huyo ni mwajiriwa serikalini na amekuwa na mzigo wa kulea watoto peke yake pasipo msaada wa mume hata pale watoto wanapohitaji kalamu au daftari kwa baba huwa hawapewi.

Baba huyo yuko radhi kwenda kunywa pombe na wanawake wa nje kuliko kuwapatia watoto madaftari na kalamu!

Wakati mwingine anapoishiwa kabisa pesa ya kunywea pombe kujifanya kuwa presha imepanda anahitaji kupelekwa hospitali.

Bila kufikiria mke pesa atapata wapi, humlazimisha ampeleke hospitali kwa lazima tena na matusi juu eti ``mwanamke gani mwenye roho mbaya namna hii, unayeshindwa kunipeleka hospitali wakati naumwa?

Una kazi ya kununua nguo mpya kila siku na kula machipsi huko kazini kwako, ndio maana unanenepeana tu, huna haya wakati nimekondeana?``

Masikini mama wa watu mwili wake ni ile miili inayostahimili matatizo kwani umwonapo amependeza sana.

Hali kadhalika hata wifi na wakwe wamediriki kumsema kwamba ananenepeana wakati kaka yao (ndugu) amekondeana.

Ndugu za mume wamemlazimisha mama huyo kumpa hati ya nyumba mume huyo kwa madai kwamba mwanamke hana ubavu wa kumiliki mali yoyote bali mmiliki hahali wa nyumba ni mwanaume pamoja na kwamba mama ndiye aliyeijenga wakati baba anajichana na makahaba katika kumbi mbalimbali za starehe.

Mama huyo alipolifikisha suala hilo kwenye vikao vya kifamilia ili lijadiliwe alionekana mbaya anayemdhalilisha mumewe kwa madai kwamba hakupaswa kumficha mume wake hati ya nyumba.

Lakini anachodai ni kwamba nyumba amewajengea watoto ili wapate mahali ka kulala na kwa kuwa anamjua mumewe akili zake zilivyo (kwa kuzingatia kwamba nyumba hiyo hakuchangia hata senti tano) hatoona uchungu kuipiga mnada na kuwaacha watoto wakitangatanga.

Kwani baba huyo yeye anachojua ni kuzaa tu kulea kwake mwiko!

Mama alipolazimisha apewe kibali cha kwenda mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake na kumjua mwenye haki, ndugu waliamua kuliingilia kati na kumshauri baba huyo atafute kiwanja kingine wajenge pamoja na mama huyo ili kuondoa mzozo uliopo sasa.

Lakini baba huyo amekuwa kinyume na ushauri wa ndugu wa pande mbili. Yeye ni pombe na yeye, wanawake na yeye na wakati mwingine hudiriki hata kuwabaka wafanyakazi wake wa ndani.

Hata watoto au hata wake za majirani amekuwa akiwazengea bila aibu. Anapokabiliwa na wenye wake hutoa vitisho na kuwatukana.

Mama wa watu mpaka sasa hathubutu hata kuleta mfanyakazi wa ndani kwa kuogopa lawana na aibu kwani mume wake ndio kituko.

Mama huyo bado anahitaji msaada wa kisheria ili aweze kuachana na baba huyo kwani mpaka sasa hivi ndugu wote wa mume wamesusa kuja hata kusalimia pale nyumbani kwa madai kwamba wifi (mkwe) wao ana roho mbaya na anamnyanyasa ndugu yao.

Eti Anti Flora mtu kunyimwa hati ya nyumba na mkewe ambayo hukuitolea jasho ni kosa?

Kama yeye aliona kujenga nyumba ya kuishi ni muhimu kwa nini basi ajenge kwenye mabaa na Guest houses?

Mama huyu anaomba ushauri wako ili aachane naye kwani kuna siku baba huyo atamtoa roho kwa uchu wa mali kwani inavyosemekana hata kitanda na godoro wanalolalia vyote ni mali ya mama.

Asante sana mpenzi msomaji wangu. Wiki moja iliyopita niliandika malalamiko ya msomaji wetu mwingine yanayofanana na haya.

Kwa Pengine leo nikumbushe tena yale niliyomshauri, tena kupitia mwanasheria aliyebobea, Dk.Sengondo Mvungi, Mhadhiri Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 imeainisha wazi namna mgogoro wa aina hiyo unaweza kutatuliwa.

Kulingana na Dk. Mvungi, mali ya mke au mume aliyoichuma wakati kabla ya ndoa, bado inaendelea kuwa ni mali binafsi ya mhusika na siyo vinginevyo.

Mali ambayo sheria inasisitiza kuwa ni halali kwa wote wawili, yaani mke na mume ni ile iliyochumwa kwa pamoja ndani ya ndoa.

Hiyo iwe ni nyumba au mashamba au mali nyingine yoyote iliyopatikana wawili hao wakiwa tayari wameoana, ni sharti wagawane sawa kwa sawa endapo ndoa hiyo itasambaratika.

Ni matarajio yangu kwamba wasomaji wengine wa safu hii watakuwa wameelimika juu ya mgogoro wa aina hiyo.

Hata hivyo, kwa ushauri zaidi, wasiliana na Chama cha Wanasheria Wanawawake Tanzania(TAWLA) ofisi ziko Ilala karibu na Hospitali ya Amana au Chama cha Waandishi Wanawake Tanzania(TAMWA) ofisi ziko Sinza Dar es Salaam.

Kama unalo linalokutatiza kuhusu purukshani za kimaisha usisite kunikandamizia kupitia barua pepe ``mailto:flora.wingia@guardian.co.tz`` flora.wingia@guardian.co.tz
Wasalaam

1 comment:

Anonymous said...

Aisee hii habari inatia uchungu sana,mimi ningemshauri huyu Mama apige moyo knode kusimami haki yake na ya watoto wake,akilegalega huyo Mbaba atatimtia matatizoni.