Monday, May 26, 2008

Kesi ya Zombe 'kuunguruma' leo jijini Dar...


KESI ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva, inayowakabili maofisa 13 wa Polisi akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Abdallah Zombe Pichani inaanza kuunguruma leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.


Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Jaji Salum Masati ambapo ina zaidi ya mashahidi 50 wa upande wa mashitaka na wanatarajiwa kutoa ushahidi wao mahakamani hapo ikiwa wananchi wengi wana hamu ya kujua ni kitu gani kitaendelea katika kesi hiyo. Mbali na mashahidi hao pia kuna vielelezo vingi zikiwemo ripoti za daktari, ramani ya tukio, maganda ya risasi na vingine. Kesi hii inatarajiwa kusikilizwa mfululuzo mpaka Juni 13, mwaka huu.


Washitakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Septemba 28 mwaka juzi baada ya kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambako ilikuwa katika hatua za awali. Walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka juzi wakiwa katika msitu wa Pande Luisi ulioko Mbezi, Dar es Salaam walimuua kwa makusudi Bw. Ephraim Chigumbi.


Katika mashitaka mengine walidaiwa kuwa siku hiyo na wakiwa katika msitu huo waliwaua kwa makusudi, Bw. Sabinusi Chigumbi, Bw. Juma Ndugu na Bw. Mathias Lukombe ambapo walikana kutenda makosa hayo. Kwa mujibu wa maelezo ya kesi hiyo ambayo yalisomwa mahakamani hapo yalisema kuwa marehemu wote walikamatwa katika eneo la Sinza,Dar es Salaam bila ya kuwa na kurupushani ambapo askari walidai kuwa ni majambazi .


Maelezo yalisema kuwa kimsingi hawakuwa majambazi bali walikuwa ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge,Morogoro na walikuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuuza mazao yao (madini) na kupeleka watoto shule Arusha.Washitakiwa hao ni Bw. Zombe,Bw. Bageni, Bw. Makele, F5912 Noel,YP4513 Jane,D6440 Nyangerella,D1406 Mabula,E6712 Felix,D8289 Michael,D2300 Abeneth, B1321 Rashid,D4656 Rajab na D1367 Philipo.Habari na Grace Michael

No comments: