Saturday, May 17, 2008

jk awakilishwa na pinda mkutanoni misri


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiongozwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri, Dr. Abuu Zeid baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Sharm El Sheikh huko nchini Misri leo.


WAZIRI MKUU Mh. Mizengo Pinda amewasili Misri leo tayari kuhudhuria Mkutano wa Kiuchumi wa Dunia kuhusu Mashariki ya Kati (World Economic Forum on the Middle East) utakaoanza kesho.



Kwa mujibuw wa taarifa toka Ikulu, mh. Pinda anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete. Kesho atatoa mada kuhusu kupanda kwa bei za mafuta, bei za vyakula na njia za kuvutia uwekezaji nchini mara tu baada ya ufunguzi.



Mkutano huo wa siku tatu ambao mada yake kuu ni “Kujiandaa kwa Siku za Usoni” (Learning from the Future) una lengo la kuliangalia eneo la mashariki ya kati katika mwaka 2025 litakuwa linafanana vipi. Mkutano huo unaofanyika katika mji wa Sharm El Sheikh ulioko kwenye fukwe za bahari ya Shamu, utafunguliwa na Rais Hosni Mubarak wa Misri kesho Jumapili saa nane mchana.


Pamoja na mambo mengine mkutano huo ambao umegawanywa katika vipindi 52, utajadili masuala ya biashara katika mfumo wa utandawazi; uwekezaji katika siku za usoni; hali ya nishati ya baadaye duniani; vijana, elimu na mafunzo; na kuangalia changamoto za ukuaji miji likiwemo pia suala la mabadiliko ya hali ya hewa yasiyoathiri maendeleo ya kiuchumi.


Mada maalumu kuhusu eneo la Mashariki ya Kati ambazo zitajadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na Fursa zilizonazo nchi za Mashariki ya Kati katika Uchumi wa Dunia; Kuvunja Mila na Kujenga Amani; Tumaini la Umoja wa Nchi za Kimediterania, Kuandaa Miundombinu ya Mawasiliano; na Mwisho wa Falme za Kiarabu Umewadia?



Jumla ya washiriki 1,200 wakiwemo wakuu wa nchi za Kiarabu, baadhi ya wakuu wa nchi za Kiafrika, mawaziri wakuu, viongozi wa kisiasa, wamiliki wa makampuni makubwa ya kikanda na dunia, wafanyabiashara na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

No comments: