Monday, May 26, 2008

Haya haya matokeo ya Stars na Malawi !!

Na Ibrahim Bakari

TAIFA Stars ya Tanzania imeanza vibaya maandalizi yake ya kusaka tiketi ya Kombe la Dunia na fainali za Afrika mwaka 2010, dhidi ya Mauritius Jumamosi kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi, The Flames uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Stars ilichezesha wachezaji wake karibu wote wakiwamo wale wanaosakata kandanda nje ya nchi, Stars ilianza mchezo kwa kuisoma The Flames na kuitia msukosuko katika dakika za kwanza cha mchezo huo.

Uchu wa mabao ya mapema wa washambuliaji , Emmanuel Gabriel, Mrisho Ngassa, Godfrey Bonny na Nizar Khalfan uliipatia kona mbili za mapema kipindi cha kwanza, lakini hazikuwa na macho.

Dakika ya 20, washambuliaji wa Stars walizinduka na kulitia majaribuni lango la Wamalawi, lakini ukuta wao chini ya kiungo wa Wisdom Ndhlovu anayeichezea Yanga ulisimama imara na kuokoa hatari zote zilizoelekezwa kwao.

Ukosefu wa umakini uliendelea kuiathiri Stars huku Nizar akikosa bao dakika ya 47 ya mchezo huo likiwamo la dakika ya 49 ambalo mwamuzi alilikataa kwa madai ya kuchezewa rafu mchezaji wa Malawi.

Lakini, mabadiliko ya kocha Marcio Maximo aliyemtoa Athuman Idd 'Chuji' na kumwingiza Kiggi Makasi yalipunguza uhai wa kiungo cha Stars.

Upungufu huo kwa kiasi fulani uliwapa nguvu Malawi ambao waliweza kuandika bao la dakika ya 55 ya mchezo kupitia kwa Essau Kanyenda kutokana na krosi ya Moses Chavula.

Katika dakika ya 79, beki wa kati wa Stars, Salum Sued alikuwa mwokozi baada ya kupachika bao hilo la kusawazisha.

Kuingia kwa Danny Mrwanda aliyechukua nafasi ya Emmanuel Gabriel kuliweza kuipa uhai safu ya ushambuliaji ya Stars ambayo ilikosa nafasi nyingi hasa kipindi cha pili, ikiwamo mashuti ya Bonny na Nizar .

Kosa kosa hizo ziliendelea baada ya Nadir Haroub 'Cannavaro', dakika ya 86 na Henry Joseph, kukosa nafasi za wazi za kuipa ushindi timu hiyo

Katika mchezo huo vikosi:

Stars:

Ivo Mapunda, Fred Mbuna, Amir Maftah, Nadir Haroub 'Cannavaro', Salum Sued, Godfrey Bonny,Henry Joseph, Athuman Idd/Kiggi Makasi, Emmanuel Gabriel/Danny Mrwanda, Mrisho Ngassa na Nizar Khalfan

Malawi:

Valence Kamzere, James Sangara, Jacob Ngwila, Wisdom Ndhlovu, Ivis Kafoteka, Hellis Mwakasungura, Tawonga Chimodzi, Noel Mkandawire, Moses Chavula, Essau Kanyenda, Jimmy Zakazaka/Chiukepo Msowoya

No comments: