Mkapa  ajitangaza kuwa ni "Mwadilifu" 
 RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya  Tatu, Bw. Benjamin Mkapa amevijia juu vyombo vya habari nchini kwa kile  alichodai vimekuwa vikimnukuu vibaya na kupotosha ukweli wa mambo. Bw. Mkapa  alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki,katika sherehe za Jubilee ya kutimiza miaka  100 ya Usista ya Kanisa la Mtakatifu Benedict lililopo Ndanda, wilayani Masasi.  Katika sherehe hizo Bw.Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi, alitumia fursa hiyo  kukanusha habari zilizochapishwa na kutangazwa na baadhi ya vyombo vya habari  hivi karibuni kuwa ameamua kuachana na siasa na kwamba sasa anajihusisha zaidi  na masuala ya dini. Alisema kuwa hana nia ya kujihusisha na masuala ya dini  zaidi kama kuwa kiongozi wa kanisa na kwamba yeye ni muumini sawa na waumini  wengine, hivyo hakuna tofauti kati ya awali na anavyojihusisha sasa na masuala  hayo nakusisitiza kwamba vyombo vya habari vilimnukuu vibaya. "Nilikuwa Chato,  mkoani Kagera, baada ya hapo nilipitia Mwanza…niliporudi nyumbani mwanangu  akaniuliza baba siku hizi unataka kuwa kiongozi wa kidini?...Nikamuuliza  kulikoni? ...akanijibu magazeti yameandika hivyo," alisema Bw.Mkapa. "Kweli siku  ya Pili nikakuta katuni kwenye gazeti ikiwa imebeba vitabu na Biblia…sasa nataka  kuwahakikishia kuwa sitaki uaskofu wala siuhitaji…mimi ni mcha Mungu wa kawaida  kama nilivyokuwa awali” alisisitiza Rais huyo mstaafu Hivi karibuni vyombo vya  habari nchini vilimnukuu Bw. Mkapa wakati alipokuwa akizungumza na waumini wa  Kanisa Katoliki la Mtakatifu Francisco Exaveri lililopo jijini Mwanza, kuwa  ameamua kuachana na siasa na sasa anajihusisha zaidi na dini. "Enzi za mimi  kujihusisha na siasa zilikoma pale nilipokabidhi madaraka kwa Serikali ya Awamu  ya Nne mwaka 2005,” alinukuliwa Bw. Mkapa na vyombo vya habari, akiwaambia  waumini wenzake katika Ibada hiyo jijini Mwanza. Sambamba na hilo, Bw. Mkapa  aliwasifu watawa hao kwa kuinua kiwango cha elimu kwa mikoa ya Kusini na  Tanzania kwa ujumla, sambamba na jitihada zao za kuboresha huduma za afya hasa  katika kutoa tiba na elimu kuhusu ugonjwa wa ukoma uliokithiri eneo hilo. "Mimi  binafsi nawashukuruni sana maana ujio wenu una mchango mkubwa kwa kiwango cha  elimu niliyoipata ambayo imeniwezesha kuwa kiongozi mwadilifu wa nchi hii … na  haya ni matunda yenu," alisema Bw. Mkapa ambaye alisoma Shule ya Sekondari  Ndanda iliyokuwa inamilikiwa na kanisa hilo. Awali Nkuu wa wilaya hiyo, Bw. Said  Amanzi, alisema serikali inatambua mchango wa watawa hao hasa katika kuboresha  afya za jamii kwa kutoa tiba kupitia Hospitali ya Ndanda na kuahidi kuwa itapewa  ruzuku ili kusaidia uendeshaji wake.Habari Kwa Hisani Ya KLH News
No comments:
Post a Comment