Tuesday, March 11, 2008

Yatima wasifukuzwe shule kwa kushindwa kulipa karo!!

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe aliagiza kuwa wanafunzi wote yatima waliofukuzwa katika Shule ya Sekondari ya Nyerere iliyoko wilayani Mwanga, Kilimanaro kwa kukosa karo warejeshwe shuleni mara moja.

Waziri Maghembe alichukua hatua hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kiverenge, kuhusiana na kitendo cha watoto yatima wapatao wanane kufukuzwa shule kwa kukosa karo na kumwomba aangalie uwezekano wa kuwasaidia ili waweze kuendelea na masomo.

Taarifa hiyo ilimkera Waziri Maghembe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, kisha kuagiza kuwa watoto wote waliofukuzwa shule wawe wamerudishwa shuleni ifikapo jana na kumuagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiverenge, kusimamia suala hilo na kwamba uongozi wa shule hiyo uwapokee wakati utaratibu wa kuwalipia ada unafanywa.

Kitendo cha watoto hao kufukuzwa shule kinatia uchungu na pia kujenga hoja ya walimu kutokuwa na huruma kwa watoto hao ambao hawana uhakika wa kulipa karo kutokana na kufikiwa na wazazi wao.

Sote tunafahamu matatizo wanayopata watoto yatima hapa nchini, kwani hata kama wazazi wao walikuwa na uwezo kutokana na baadhi ya walezi wao kuwadhulumu haki zao, hivyo kuwazidishia uchungu maishani.

Mbali na ambao wazazi wao walikuwa na uwezo, wako ambao wazazi hawakuwa na chochote hivyo kuchukuliwa na ndugu ambao hawana uwezo kwa ajili ya kulelewa.

Ikumbukwe kuna baadi ya watu wameamua kuchukua jukumu la kuwatunza watoto yatima hata kama hawana uwezo ili waweze kuishi na linapotokea suala la elimu wanawapeleka shuleni, lakini kutokana na kutokuwa na uwezo hushindwa kulipa ada kwa wakati.

Kinachoshangaza na kusitikisha ni hatua za haraka zinazochukuliwa na walimu kuwafukuza watoto hao shule, jambo ambalo huwaumiza zaidi watoto kiasi cha kuwaathiri kisaikolojia kwa kuwakumbuka wazazi wao, hivyo kuwafanya wapoteze matumaini.

Tunaamini kuwa walimu ni wazazi wanaojua matatizo na wanaelewa fika matatizo yanayowasibu watoto yatima, hivyo hawakustahili kuwafukuza shule badala yake wangechukua hatua nyingine zinazoweza kuwahamasisha ili waendelee kuipenda.

Kitendo cha mtoto kutolipiwa karo na akijua kwamba hajalipiwa na hasa hawa watoto yatima, kwake inakuwa kero hata kama hajaulizwa wala kutishiwa na walimu kwamba atafukuzwa; na wakati mwingine huathiri maendeleo ya mtoto kutokana na imani kwamba hathaminiwi kwa vile ni yatima ndiyo maana halipiwi karo.

Kuna watoto wengine ambao hawana watu wa kuwalipia karo, hivyo walimu hao hawakutakiwa kuchukua hatua kali kama hiyo ambayo kwa watoto wa kundi hilo ni kubwa kuliko kuchapwa fimbo.

Yaliyotokea Mwanga yanatokea sehemu mbalimbali hapa nchini kutokana na walimu kuthamini zaidi malipo kuliko kuzingatia matatizo yanayowakabili watoto wa aina hiyo.

Hivi kweli watoto wanane wanaleta hasara kiasi gani kwa shule kama walimu wataamua kuwasaidia kutokana na matatizo yao ya kuwa yatima? Mbona katika baadhi ya shule kuna watoto wa walimu wanaosoma bure ingawa wana uwezo? Si bora zaidi kuwasaidia watoto ili iwe kama sadaka ya shule hiyo?

Tunawaomba wamiliki na walimu wa shule zote nchini kutochukua hatua haraka kuwafukuza watoto yatima mpaka wahakikishe kuwa karo haikulipwa kwa makusudi au mwanafunzi alipewa karo lakini akaitumia.

No comments: