Wednesday, March 12, 2008

Ufisadi sio ajali ya kisiasa

Na Haji Mbaruku

Vitendo vya ufisadi vilivyoigubika nchi ambavyo hata hivyo mjadala wake bado haujaisha, vimepewa sura mpya kuwa ni ajali za kisiasa.

Professa mmoja wa siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam aliwaambia wanafunzi wake hivi karibuni kuwa watafsiri msemo huo ikiwa ni kweli ufisadi ni ajali ya kisiasa.

Kwani ajali ni nini? Ajali sio kitu cha makusudi. Ajali inatokea kwa bahati mbaya tu. Kwa hiyo ajali ni tukio la bahati mbaya.

Katika ajali kuna kufa na kupona.Hakuna dereva anayependa kukatika mguu wake ama mkono hata kama aliisababisha ajali hiyo kwa makusudi.

Lengo lake lilikuwa ni kufika haraka ndio maana akakumbwa na ajali.

Sasa kama ikiwa ajali ni kitu cha bahati mbaya, hatuwezi kusema ufisadi ambao kwa tafsiri yake nyingine ni zaidi ya rushwa haiwezi hata kidogo kutafsiriwa kuwa ni ajali.

Taifa lilikumbwa na tatizo la uhaba wa maji ambao ulisababisha tatizo la umeme.

Ukafanyika mpango wa kuileta kampuni ya umeme ili iweze kuzalisha umeme kwa mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo, pamoja na kutetewa sana kuwa Richmond ilikuwa safi, wajuzi wa mambo walijua kuwa ipo siku ukweli utajulikana kwa sababu kwenye ukweli uongo hujitenga.

Ukweli ulipatikana na uongo ukajitenga. Sasa watanzania tunapolazimishwa tuwaambie wenzetu kuwa sakata la Richmond lilikuwa ni tukio la bahati mbaya, tunapata mashaka na viongozi wetu.

Tunafahamu kuwa kidiplomasia, unaweza kumtetea mtu kwa kusema ni ajali lakini katika masuala ya siasa sijaona mahali wanasayansi wa siasa wakizungumzia ajali za kisiasa.

Wanasayansi wa masuala ya siasa kama vile Robert Eyestone, Thomas Dye, David Easton, Wilson Woodrow hawajawahi kuandika mahali popote pale ajali za kisiasa ni zipi.

Umefika wakati kwa watanzania sasa kupima uwezo wa viongozi wetu badala ya kuendelea kushabikia mambo yanayodidimiza maendeleo ya nchi hii ambayo kwa miaka 47 sasa, inaendelea kuitwa nchi ya dunia ya tatu.

Tangu hayati Mwalimu Julius Nyerere alipotangaza maadui wetu watatu kuwa ni ujinga, umaskini na maradhi, hakuna hata adui mmoja kati ya hao aliyefanikiwa kumshinda mwenzake.

Wapo watu wachache wanaonufaika kupitia kwa wengi. Sasa tunapowabaini watu wanaodidimiza nchi hii na kutusababishia mzigo mzito mbele ya safari na kisha tukawawajibisha, tunawapoza kwa kusema ni ajali.

Mama Anne Kilango Malecela alizungumza vizuri bungeni. Kwa sababu ripoti ile aliisoma na ndio maana aliwaambia wabunge wenzake kuwa hakulala jana yake.

Mambo yote yaliyoashiria kuwa kulikuwa na ufisadi mle.Hakutajwa mtu kwa kusingiziwa ama kutaka kudhalilishwa.
Dk. Harrison Mwakyembe ni mwanasheria.

Ameshafundisha Chuo Kikuu kwa muda mrefu. Ameshatunga vitabu vingi. Vingi vinasomwa na wanafunzi wa Elimu ya juu.

Dk.Mwakyembe anajua madhara ya kumsingizia mtu. Anajua madhara ya kusema uongo. Kwa sababu kisheria makosa yote hayo yanaangukia kwenye kesi za jinai.

Yaani kazi yoote iliyofanywa na Dk.Mwakyembe na wajumbe wenzake haitakuwa na maana, basi kama ufisadi ule uliotokea utafananishwa na ajali za kisiasa.

Mi nadhani tuwe wakweli. Kiongozi mzuri ni yule anayesema ukweli. Kiongozi mzuri ni yule asiyekuwa na majungu, hana uoga katika kusimamia ukweli.

Afrika leo hii yawezekana haina viongozi wanaofanana au kukaribia ukweli wa viongozi shupavu watangulizi wenye sifa ziliozotukuka akina Kwame Nkrumah, Leopold Senghor na Patrice Lumumba .

Viongozi wengi wa leo ni kama hawana itikadi wala falsafa sahihi zinazotuelekeza kwenye maendeleo yaliyo ya kweli.

Watu wameshazungumza sana kuhusu kiongozi wa juu kabisa kufanya biashara Ikulu. EPA, Richmond, IPTL zote zinamhusu yeye. Lakini tunalazimishwa kuchukua haatua za kumuacha apumzike.

Sasa tukisema kuwa kila anayefanya ufisadi nchi hii aachwe apumzike, itakuwaje.

Watu wanapolilia kutungwa kwa Katiba mpya ambayo itaondoa ukiritimba huu wa Rais anapomaliza muda wake kutoshtakiwa wanaonekana hawana maana hata kidogo na kwamba wametumwa!.

Watanzania wanahitaji elimu ya uraia kwa kiasi kikubwa sana. Hasa watu wa vijijini.

Leo hii hawana habari kuhusu suala la Richmond, wanasikia sikia tu kwa juu lakini hawapati undani wa jambo hili.

Leo hii nchini Cameroon, wananchi wa nchi hiyo wamelazimika kuandamana nchi nzima kupinga kupanda kwa bei ya mafuta.

Kupanda kwa bei ya mafuta kumewaumiza sana na sasa hawaoni sababu ya kuendelea na Rais Paul Biya.

Yawezekana nchi yetu isifikie huko lakini angalau kuchukua hatua muafaka kushinikiza mambo yanayoelekea kuwa ni mzigo usio na sababu kwa wananchi wengi.

No comments: