Thursday, April 29, 2010

Cuba kujenga kiwanda cha madawa nchini!!!

SERIKALI ya Cuba imeanza kufuatilia utekelezaji wa ahadi yake iliyotoa kwa serikali ya Tanzania kuhusu ujenzi wa kiwanda cha madawa nchini.

Akizungumza na Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, Mkurugenzi wa maabara ya kibaiolojia na dawa ya Cuba, Dk. Jose Antonio Fraga Castro amesema wamepanga programu ya ujenzi wa kiwanda hicho ifanyike katika kipindi cha miaka miwili hadi miwili na nusu.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana, Dk Castro alieleza kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni kuitikia mwito wa Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais walipotembelea maabara ya Labiofam kwa nyakati tofauti nchini Cuba ambapo waliomba Cuba isaidie jitihada za kudhibiti malaria nchini.

Alisema kiwanda hicho kitatengeneza dawa kwa kutumia njia za kibiolojia bila ya kutumia dawa za kemikali ambazo mara nyingi huharibu mazingira.

Alisema pamoja na kutengeneza dawa ya kudhibiti malaria kiwanda hicho kitatengeza pia dawa za chanjo kwa wanyama pamoja matumizi ya tekinolojia ya kisasa katika kilimo na kufanya shughuli za utafiti.

Dk. Castro alisema wakati mchakato wa kujenga kiwanda hicho ukiwa mbioni wataanza haraka iwezekanavyo na mradi wa majaribio wa kuangamiza mazalio ya mbu kwa kutumia dawa hiyo isiyo na kemikali kwa mkoa wa Dar es salaam.

Kwa upande wake Makamu wa Rais alimueleza Mkurugenzi huyo kuwa serikali ya Tanzania imedhamiria kutokomeza malaria na mwezi mmoja uliopita Rais Kikwete alizindua mradi mkubwa wa malaria wenye kauli mbiu ‘malaria haikubaliki’.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais alikutana na Balozi wa Afrika Kusini nchini Phanduyise Henry Chiliza ambapo walizungumzia kwa ujumla changamoto za kiuchumi katika bara la Afrika.

No comments: