Thursday, June 18, 2009

KUTANA NA ALBINO FULANI

BABU SIKARE A.K.A ALBINO FULANI

Babu Sikare si jina geni mjini Columbus Oh ni kijana machachari mwenye mbwembwe na ucheshi na kipaji kikubwa cha kughani na kutawala jukwaa ambacho kinajulikana na wachache, yeye ni mzaliwa wa Daressalaam nchini Tanzania.

Amezaliwa na ulemavu wa ngozi (Albino) lakini si wengi wanaotambua hali hiyo kwani wengine wanadhani yeye ni “mzungu” lakini hilo halimzuii kuonyesha cheche zake wala kufurahia maisha yake.

Babu Sikare aka Albino Fulani ameamua kupambana na mauaji ya Albino Tanzania akiwa amekulia Dar na kusoma Oysterbay Primary, anasema anakumbuka wenzake walikuwa wakitemea mate mashati yao ili wasigeuke Albino wakati alipokuwa shule ya msingi na kitu ambacho kamwe hatasahau ni kitendo kama hicho kufanywa na mwalimu wake!

Hivyo akiwa amehamia Marekani kiasi cha takriban miaka sita na nusu iliyopita kwa masomo ameguswa mno na hali ya mauaji nchini Tanzania na Burundi na hivi sasa anafanya juhudi za kupambana kuokoa maisha ya wenzake hao na ameamua kutoa single ya kwanza iitwayo “Barua kwa Mama” hii ni kisa cha kweli baada ya kumpoteza mama yake mzazi hayati Grace Mwasi Sikare.

Albam yake kamili bado iko jikoni inapikwa hapa Marekani na anashirikiana na wanamuziki kama vile Mkali Fulani, Mtaalam Fulani, Chid Benz na Tinted pamoja na mambo mengine ya maisha ya kila siku album hii itaelezea maisha ya Albino kuwa ni sawa na watu wengine wa kawaida.

Single yake hiyo itazinduliwa Columbus Oh 20/06/09 katika ukumbi wa Boomerang. Wadau wa Columbus, Indiana, Michigan na vitongoji vyake mnakaribishwa sana.

Wakazi wa Dar na vitongoji vyake wajiandae kwani Babu Sikare anategemea kutoa albamu yake Tanzania mwezi Julai ambayo itakuwa na nyimbo 9 na itakwenda kwa jina hilo hilo la kwake “Albino Fulani”.


No comments: