Wahariri  wamweka kitanzini 
 Mkuchika  
Hatua ya Waziri wa  Habari,Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, ya kulifungia gazeti la  MwanaHalisi, imepingwa vikali na wahariri, ambao wamepitisha maazimio saba  kuhusu hatua hiyo, likiwamo la kutoandika na kutangaza habari na picha yoyote ya  matukio yanayomhusu waziri huyo kwenye vyombo wana vyovisimamia.
 Wahariri hao, pia wameazimia  kumwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kumuasa afikirie upya uteuzi wa Mkuchika  kuongoza Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, kutokana na maamuzi yake  yanayohusu taaluma ya habari nchini, ambayo yameonyesha kuwa hana uwezo wa  kuongoza wizara hiyo. Vilevile, wameazimia kuishitaki serikali kwenye Jumuiya ya  Kimataifa na nchi wafadhili namna inavyovunja misingi ya utawala bora kwa  kuminya uhuru wa vyombo vya habari; kufanya maandamano kwenda wizarani hapo  kuwasilisha tamko kuhusu Mkuchika anakoipeleka taaluma ya habari nchini.  
 Wahariri hao pia, wameazimia  kwenda mahakamani kuomba uamuzi wa Mkuchika kulifungia MwanaHalisi ubatilishwe  na wamewataka watu wote wenye malalamiko yanayohusu taaluma ya habari,  wayapeleke kwenye Baraza la Habari Tanzania (MCT) au kwenye Jukwaa la Wahariri  au mahakamani. Maazimio hayo yalipitishwa kwa kauli moja na wahariri hao katika  kikao chao cha pamoja, kilichofanyika katika Hoteli ya New Africa, jijini Dar es  Salaam jana. 
 Kikao hicho kiliandaliwa na  Jukwaa la Wahariri na kiliongozwa na Mwenyekiti wake, Sakina Datoo. Wahariri  hao, wamefikia maazimio baada ya kujiridhisha kwamba, hatua ya Mkuchika  kulifungia MwanaHalisi, sababu alizozitaja na matukio mengine ya nyuma  aliyoyafanya kuhusu taaluma ya habari, imeonyesha kuwa ana upungufu mkubwa  katika taaluma ya sheria, mbinafsi, si muadilifu, mbabe, mwenye hasira na  anaiaibisha serikali ndani na nje ya nchi. Wahariri hao walisema kwamba suala la  maudhui ya habari ya MwanaHalisi kama imezingatia vigezo vya taaluma. linaweza  kujadiliwa na jukwaa hilo. 
 Walisema kwamba kimsingi,  serikali haiwezi kuwa mlalamikaji, hakimu na bwana jela katika shitaka lake  yenyewe, ndiyo maana wanaamini kwamba kama kuna malalamiko yoyote yawasilishwe  kwenye vyombo husika ili haki iweze kutendeka. Vyombo vya habari vilivyoridhia  maazimo ya jana ni pamoja na Nipashe, The Guardian, Guardian on Sunday, Tanzania  Daima, Mtanzania, The African, The Express, Majira, Kulikoni, ThisDay,  Mwananchi, Citizen, Changamoto.
 Vingine ni ITV na Radio One, Star  Tv, BBC na Channel Ten. Wahariri wa vyombo hivyo walisema kwamba kuanzia leo,  habari zozote zinahusu Mkuchika hazitatolewa kwenye vyombo wanavyoongoza. Hatua  kama hizi, ziliwahi kuchukuliwa dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,  Ramadhani Omar Mapuri na Jeshi la Magereza kutokana na tukio la kushmabuliwa  mpiga picha. Jumatatu wiki hii, serikali ililifungia gazeti la Mwanahalisi kwa  muda wa miezi mitatu kwa madai ya kuandika habari mbaya ya kumdalilisha  Rais.Habari Kwa Hisani Ya  Nipashe.
 
No comments:
Post a Comment