Wednesday, September 10, 2008

KUMEKUCHA; BBC KWENYE UCHAGUZI USA!



Shirika la utangazaji la Uingereza, BBC, kupitia Idhaa zake mbali mbali ikiwemo ya Kiswahili(bbcswahili.com), litafanya msafara wa basi maalum litakalopita kwenye majimbo mbali mbali ya Marekani katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu - safari inaanza tarehe 10 Septemba (leo) huko Los Angeles na itamalizika ifikapo Oktoba 17 jijini New York.

Safari hiyo itakayodumu siku 38, itaanzia kwenye pwani ya magharibi ya Marekani,ambako mojawapo ya mada zitakazofanyiwa kazi ni kuangalia ushawahishi wa utamaduni wa kimarekani duniani.Basi hili la kisasa lililofanyiwa marekebisho kuhudumia waandishi 12 kwa wakati mmoja, limepambwa maandishi ya BBC pamoja na yale ya uchaguzi wa Marekani 2008.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Hassan Mhelela, atajiunga na basi ifikapo tarehe 12 Oktoba katika mji wa Akron kwenye jimbo la Ohio.Kwa muda wa siku tano atakuwa safarini mpaka mwisho jijini New York ambako msafara utakamilika kwenye viwanja vya Times Square wakati waandishi kutoka vyombo vya habari vya Marekani kama ABC, NBC na CBS watawahoji waandishi wa BBC kuhusu safari yao na kuhitimisha mjadala.Mhelela atakuwa Marekani mpaka kukamilika kwa uchaguzi mwezi Novemba.

Lengo la safari hii ni kuweza kupata mtizamo wa wapiga kura katika maeneo ambayo kwa kawaida waandishi wa vyombo vya kimataifa huwa hawafiki kuwasikiliza wapiga kura.Je yale yanayoandikwa na vyombo vya Marekani ndiyo yanayowagusa wananchi?Safari hii itajaribu kupata majibu.

Waandishi wa BBC wakiwemo waliobobea katika fani za redio, tovuti na televisheni, watakuwa wakifanya kazi na kulala ndani ya basi hili ambalo pia litakuwa limebeba vifaa vya kisasa vya kuandaa na kurushia matangazo kutoka sehemu yoyote wakati wa safari itakayopita katika maeneo ya vijijini pia.Kwa ujumla maswala yatakayopewa kipaumbele ni hali ya uchumi, sera za mambo ya nje, umuhimu wa kuwa na mgombea mwenye asili ya Afrika kwa mara ya kwanza (Barack Obama) na pia kuibuka kwa mwanamama Sarah Palin kama mgombea wa kiti cha makamu wa rais.

Waandishi katika msafara huu watahudhuria mdahalo wa pili wa wagombea urais utakaofanyika tarehe 15 Oktoba huko Hempstead, Long Island ambapo Barack Obama wa Democratic atatoana jasho na mkongwe John McCain wa Republican.

Mpaka kukamilika kwake basi litakuwa limesafiri takriban kilometa 6,500 na kupitia majimbo yapatayo 15.Kila mwandishi atakuwemo ndani ya basi kwa siku zisizopungua tano kabla ya kushuka na kupisha mwingine.Jumla ya waandishi 44 watakuwa wameingia na kushuka kufikia mwisho wa safari Oktoba 17.

Wadau wenye kufuatilia siasa za Marekani mnakaribishwa kushiriki kwenye mijadala na mahojiano yatakayokuwa yakifanywa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC mpaka baada ya uchaguzi Novemba 4.Kupata fursa ya kushiri unaweza kutuma ujumbe kwa barua pepe, swahili@bbc.co.uk au tuma sms kwenye nambari:+ 44 7786 202 005.

No comments: