Tume ya Muhimbili Yatajwa..
Waziri wa Afya Profesa David Mwakyusa akimjulia Hali Mmoja wa majeruhi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam juzi baada ya Mgonjwa wa akili Bw David Denge(21) kushambulia wagonjwa wenzake na Kuua wawili.
----
SERIKALI imeunda Tume maalumu ya wataalamu watano kuchunguza tukio la mauaji lililofanywa na mgonjwa wa akili Jumatatu wiki hii katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH) Dar es Salaam.Agosti 11,mwaka huu,mgonjwa wa akili David Denge(21),aliyekuwa amelazwa Muhimbili akitokea Hospitali ya Mwananyamala,Kinondoni, aliwaua wagonjwa wenzake wawili wa akili na kuwajeruhi wengine watano kwa chuma kinachotumika kutundika chupa ya kuongezea maji mwilini.
Tume hiyo inayoanza kazi Jumatatu ijayo,imepewa wiki mbili kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na itafanya kazi chini ya Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara hiyo ambaye atahakikisha Tume inapata msaada unaohitajika.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam,Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Profesa David Mwakyusa alisema Wizara imeunda tume hiyo ili kubaini mazingira yaliyochangia kutokea kwa tukio hilo na kisha kutoa taarifa kwa umma na mapendekezo ya kuzuia tukio hilo lisirudiwe,
Alisema tume hiyo itakuwa na wajumbe watano ambao wawili watatoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao ni Dk.Joseph Mbatia na Jovin Lyimo,Nassoro Mnambila kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,Joviter Katabaro kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mjumbe mwingine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye jina lake litapatikana baadaye.
No comments:
Post a Comment