Wednesday, April 13, 2011

Vurugu la Leo Bungeni Mjini Dodoma''Hatoki Mtu,Tutatoka Wote''

Huenda leo Bunge la Tanzania lingeingia kwenye orodha ya viroja vya Wabunge wa Mabunge (kama haya, bofya hapa utizame vidoe Youtube) ya nchi mbalimbali Duniani kupandwa jazba kiasi cha kujikuta (pasina kufahamu) wanageuza kumbi za Bunge kuwa viwanja vya 'ndondi', mieleka, karateka, kulengana-shabaha, michezo ya kujificha, mipasho, na mengineyo.

Leo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Anne Makinda wakati anaongoza kikao cha uchaguzi wa wajumbe kwenye taasisi mbalimbali za kibunge ilimbidi afikie hatua ya kuwaambia Wabunge kuwa 'walikuwa wanafanya mambo ya kijinga' kutokana na mabishano yaliyokuwa yakiendelea baina ya wabunge hao.


Ubishi ulizuka pale Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje, CHADEMA, alipotamka Bungeni kuwa utaratibu wa kuwapata wagombea wa nafasi hizo za wajumbe wa taasisi mbalimbali ulifanyika katika "dark market", na ndipo Wambunge kutoka CCM walipomshinikiza Mbunge huyo aifute kauli yake hiyo.


Wenje alipoma kufuta kauli, ndipo mabishano yaliendelea zaidi huku baadhi ya Wabunge wakisema, 'out, out, out', wengine wakatamka 'akanywe kikombe cha Babu' na 'toka nje'.
Wengine wakasema, "Mnatumia wingi wenu kutuburuza" "Mmezowea kutuburuza" "Tufunge mlango tupigane” (sikiliza audio)
Spika Makinda kwa mara nyingine aliwakumbusha wabunge kuwa wanatizamwa na wananchi waliowachagua, akamtaka Wenje kuifuta kauli yake na kuwataka wabunge wengine kukaa kimya ili kumpa nafasi Mbunge Wenje aliyesimama kuzungumza azungumze. Licha ya kauli ya Spika, wabunge waliendelea kuzungumza bila utaratibu na kusababisha 'zogo' hilo kuchukua dakika 10.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alimweleza Spika kuwa ulikuwa wakati muafaka kwa yeye kumwamuru Wenje atoke nje ya Bunge.


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, CHADEMA, akasema kwambaKamati ya Uongozi ya Bunge ilikutana kuzungumzia suala hilo, lakini hazikutolewa fomu ili wagombea wajaze. Akasema pia kuwa kamati hiyo si "dark market" lakini haikuwa sahihi kuitafsiri visivyo kauli ya Wenje, wao (wabunge) wote ni wanasiasa, wawe na ngozi ngumu.


Bado baadhi ya wabunge wakaendelea kusisitiza kuwa Wenje atoke, Zitto akawajibu kuwa hatoki, na wabunge wengine wakasema “hatoki mtu, tutatoka wote”


Kwa mara nyingine tena Spika Makinda akampa Wenje fursa ya kufuta kauli yake, ndipo Mbunge Wenje akafafanua kuwa hakusema Kamati ya Uongozi ni "dark market", ila alimaanishautaratibu uliotumika. Mwishowe akasema, anafuta maneno "dark market", na kuweka "white market" badala yake.

No comments: